Magufuli apokea ujumbe wa kamisheni ya amani AU

Rais John Magufuli

Muktasari:

Tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya Tanzania na Misri imekutana kuainisha maeneo yenye fursa na yanayopaswa kufanyiwa kazi.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amefanya mazungumzo na kamishna wa amani na usalama wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Balozi Smail Chergui aliyewasilisha ujumbe wa mwenyekiti wa kamisheni hiyo, Moussa Faki Mahamat.

Chergui amesema leo Aprili 20, 2018 katika mazungumzo na Rais Magufuli yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Ikulu imesema viongozi hao wawili wamejadili masuala ya amani na usalama barani Afrika na hasa ukanda wa maziwa makuu.

Amesema pia wamejadili masuala ya wakimbizi, huku akimshukuru Rais Magufuli kwa ushauri, mchango wa mawazo na uzoefu katika kuimarisha amani na usalama.

Wakati huohuo, Rais Magufuli amekutana na msaidizi wa Rais wa Misri na waziri mkuu mstaafu wa nchi hiyo, Ibrahim Roshdy Mahlab aliyewasilisha ujumbe kutoka kwa Rais wa Taifa hilo, Abdel Fattah el-Sisi.

Baada ya mazungumzo, Mahlab amesema wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Tanzania na Misri, ikizingatiwa kuwa zipo fursa nyingi ambazo nchi hizi mbili rafiki zinapaswa kuzifanyia kazi.

Mahlab amebainisha kuwa utekelezaji wa makubaliano yaliyowekwa wakati wa ziara ya Rais wa Misri, Abdel Fattah el-Sisi nchini umeanza ambapo tume ya pamoja ya ushirikiano kati ya nchi hizi imeshakutana nchi Misri na kuainisha maeneo yenye fursa na yanayopaswa kufanyiwa kazi.