AfDB yaridhishwa utekelezaji miradi ya nishati

Muktasari:

Rais AfDB afananisha umeme katika maendeleo sawa na damu mwilini mwa binadamu.

Dodoma. Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dk Akinumwi Adesina amesema benki hiyo imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya nishati nchini, ambayo inachochea mageuzi katika maisha ya wananchi.

Akizungumza baada ya kuwasili mkoani Dodoma Aprili 26, 2018 na kutembelea kituo cha kupoza umeme cha Zuzu, amesema benki hiyo inatambua na kupongeza juhudi za  Serikali katika kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.

“Ujenzi wa kituo cha kupoza umeme ni mkakati wa Serikali wa kuondoa changamoto ya upatikanaji nishati ya umeme kwa wananchi na umelenga  kupunguza tatizo la upatikanaji wa umeme katika nchi jirani zinazopakana na Tanzania zikiwamo Burundi na Kenya,” amesema.

Amesema benki hiyo imetoa Dola 75 milioni  za Marekani kufanikisha mradi huo wenye thamani ya zaidi ya Dola 220 milioni.

"Umeme ni muhimu katika maendeleo ni sawa na damu katika mwili wa binadamu, ukiwa na damu mwilini unakuwa hai kama huna unakufa. Kwa hiyo uchumi bila umeme wa uhakika hauwezi kushamiri," amesema Dk Adesina.