Gari la JWTZ lapata ajali

Kamanda wa Polisi, mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei

Muktasari:

Askari sita wa JWTZ walijeruhiwa na kukimbizwa hospitali.

Morogoro. Gari la askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wametoka katika sherehe za miaka 54 ya Muungano Dodoma, limepata ajali baada ya kuigonga gari aina ya Noah na kusababisha vifo vya watu wawili.

 Waliofariki, ni waliokuwa kwenye Noah, akiwamo mtoto miezi tisa, Amina Hassan na dereva wa Noah, Zindao Cornell, askari wa JWTZ.

 Akizungumza na MCL Digital leo Aprili 27, Kamanda wa Polisi, mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amesema gari lililokuwa limebeba askari wa JWTZ, lilipata hitilafu katika tairi na kuigonga Noah.

“Ni tatizo la kiufundi, kwa sababu gari lililobeba wanajeshi lilipata hitilafu ya kukakamaa kwa tairi la mbele, gari hilo likamvuta dereva upande wa kulia na  likagonga Noah,” amesema.

Amesema askari sita wa JWTZ, walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.

 Kadhalika ameongeza kuwa mama mwenye mtoto wa miezi tisa, amelazwa katika hospitali hiyo.