Thursday, May 17, 2018

Mbunge Chadema ataka kuifadhili Wizara baada ya Serikali kushindwa kuipa fedha

Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha akizungumza

Mbunge wa Serengeti, Marwa Chacha akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi 

By Habel Chidawali, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Mbunge wa Serengeti (Chadema), Marwa Chacha amesema yuko tayari kuifadhili Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikiwa Serikali imeshindwa kuisaidia wizara hiyo.

Akizungumza katika mjadala wa bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi Mei 17, 2018, Chacha amesema wizara hiyo ni hewa  na imeundwa kwa ajili ya kunufaisha wachache.

“Nimesoma katika kitabu ukurasa wa nane, mwaka jana mlitengewa fedha za maendeleo Sh 4bilioni, lakini hadi mwisho mlikuwa mmepewa sifuri, huku ni kuwadhihaki wafugaji na wavuvi. Kama Serikali imeshindwa kuwapa fedha za maendeleo, niko tayari njooni niwafadhili,” amesema Chacha.

Wizara hiyo leo imeliomba Bunge kuidhinishia Sh56.45 bilioni katika bajeti yake ya mwaka wa fedha 2018/19, huku ikieleza kuwa fedha za maendeleo za bajeti yake ya mwaka 2017/18, hadi kufikia Aprili 2018, zilikuwa hazijapokewa.

Kati ya fedha hizo, Sh 4bilioni ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo katika sekta ya mifugo na Sh2bilioni kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya uvuvi.

 

 


-->