RIPOTI MAALUMU: Sugu ajifananisha na mfungwa wa kisiasa

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema baada ya kufika katika ofisi za chama hicho Kanda ya Nyasa zilizopo eneo la Kadeghe jijini Mbeya, muda mfupi baada ya kuachiwa huru kufuata kifungo cha miezi mitano. Picha na Maktaba

Mbeya. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amejifananisha na mfungwa wa kisiasa huku akidai kuwa alijua anakwenda kufungwa hata kabla ya kesi kwenda mahakamani kwani dalili zilianza kuonekana wakati akihojiwa polisi.

Sugu na katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walifungwa kifungo cha miezi mitano kuanzia Februari 26 mpaka Mei 10 mwaka huu, katika Gereza Kuu la Ruanda baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya kuwakuta na hatia ya kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.

Sugu na Masonga walidaiwa kutoa kutamka maneno hayo ya fedheha kwa Rais Magufuli Desemba 30, mwaka jana, wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge jijini hapa.

Sakata la kesi hiyo lilianza Januari 2 mwaka huu, baada ya Sugu na Masonga kuitwa ofisi ya Mkuu wa Upelelezi (RCO) Mkoa wa Mbeya na wote wawili kuhojiwa kutokana na maneno waliyoyatoa kwenye mkutano huo.

Katika mahojiano maalumu na Mwananchi ikiwa ni mwendelezo wa mahojiano maalumu, Sugu amedai yeye na Masonga walitambua wazi kuwa kuna mazingira ya kufungwa tangu hatua ya upelelezi.

“Tulikuwa tunajua kuna kufungwa… kwanza tangu mwanzo tunaitwa polisi kwa RCO, tulijua…..hii ilinifanya nijue kuna shinikizo tu dhidi yangu,” anasema mwanamuziki huyo wa muziki.

“Hata mwenendo wa kesi yenyewe ulikuwa unaonekana wazi kabisa lazima tufungwe, hivyo tulijua kabisa kulingana na mazingira yalivyofanya vile. Na hata hatua ya hakimu kutunyima dhamana na kulazimika kukaa mahabusu katika gereza kuu.”

Mwanasiasa huyo anasema baada ya kukaa mahabusu siku 24 akiwa na Masonga kabla ya kutoka kwa dhamana, waliacha vitu vyao vyote gerezani (nguo na vyombo vya chakula) na siku moja baadaye alirudi gerezani kwa ajili ya kuwaona na kuwasalimia wafungwa aliokuwa akiishi nao.

Sugu anasema baada ya kufika gerezani hapo wafungwa walitaka kumpatia vitu vyake alivyoviacha, lakini aliwaeleza waviache kwani kuna kurudi tena gerezani.

Anasema, “Nilijua hivyo sikuona umuhimu wowote wa kuvichukua vitu vyangu, hivyo niliwaambia viacheni tu ila mnitunzie na nitavikuta kwa sababu tutarudi tena.”

Ajitaja mfungwa wa kisiasa

Sugu anasema anaamini kwamba yeye alikuwa ni mfungwa wa kisiasa licha ya kuhukumiwa kwa kosa la jinai, lakini hilo kosa anadai alitafutiwa kwa sababu za kisiasa.

“Ukishakuwa mfungwa wa kisiasa, kosa lazima utapewa. Mimi nilipewa kosa la kumfedhehesha Rais, lakini ikumbukwe hata Rais Mandela (Nelson Mandela wa Afrika Kusini) alipewa kosa la ugaidi, sasa wakati Mandela anakwenda kufungwa kweli alikuwa gaidi? Obasanjo wa Nigeria naye alipewa kesi ya uhaini akahukumiwa kunyongwa, lakini baadaye akawatoka na mwisho wa siku akaja kuwa Rais wa nchi ya Nigeria.

“Kwa hiyo mfungwa wa kisiasa unaweza ukapewa kosa lolote lile lakini sababu iliyopo nyuma yake zinakuwa ni za kisiasa. Tangu lini kumfedhehesha mtu ikawa ni kosa la jinai? Kumfedhehesha mtu ni kosa la madai. Kwa hiyo hapa kifungo walichotufunga na kosa walilolisema ni vitu viwili tofauti. Na ndio maana tukakata rufaa kupinga hukumu na kifungo kile na tunasisitiza kwamba tulifungwa kibatili na tuliachiwa kibatili,” anasema.

Asema hajayumba

Akizungumzia hatua ya kufungwa jela na msimamo wake, Sugu anasema kufungwa kwake kumemfanya awe jasiri zaidi kuliko alivyokuwa huko nyuma na kumuongezea ari ya kusimamia ukweli anaouamini.

Anasema, “kikubwa tu ni kwamba wajue sijateteleka, wala sijapunguza ari ya moyo wa kuwatumikia wananchi wangu… nipo vizuri na imara zaidi na kitendo cha kuniweka ndani kimenipa ‘experience’ (uzoefu) zaidi, nimejua matatizo, nimeitafakari hali ya Mbeya na hali ya nchi kwa ujumla nikiwa ndani.”

“Lakini kwa watesi walionifunga waondoe hofu, wasiniogope kwani wanaonekana wana wasiwasi na hofu sana na Sugu, Mbeya ni jiji la amani na kabla hawajasimamia mchakato wa kunifunga wanazunguka mitaani na kufurahia maisha, lakini sasa baadhi yao wanakuja kwangu. Kwa hiyo niwahakikishie tu kwamba hakuna mwenye kinyongo dhidi yao, wala wasiniogope Sugu wala wasiwaogope wana Mbeya.”

Sugu anasema baada ya kufungwa, alitoa wito kwa wananchi wake kwamba wawe watulivu na wasifanye jambo lolote lile na bahati nzuri walimuelewa na wakawa watulivu hadi alipotoka alikuta hali ya amani imetawala.

Anasema anaamini kuwa alifungwa kwa sababu za kisiasa, hivyo alitarajia baada ya kufungwa kwake kungesaidia kuleta maendeleo kwa wapinzani wake ndani ya Jiji la Mbeya, lakini hadi ametoka hakuna alichooona kimebadilika.

Itaendelea kesho.