Serikali yawataka waajiri kujiungana WCF

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Stella Manyanya

Muktasari:

Manyanya amesema hali hiyo itawanufaisha  wafanyakazi wanapoumia kazini kutokana na majanga mbalimbali.

Dodoma. Serikali imeagiza kwa waajiri wote nchini kujiunga Katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ulioanzishwa hivi karibuni na sheria yake kupitishwa na bunge.

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Stella Manyanya amesema hali hiyo itawanufaisha  wafanyakazi wanapoumia kazini kutokana na majanga mbalimbali.

Waziri Manyanya ameyasema hayo leo Mei 18, wakati akijibu swali la Lathifa Chande Mbunge wa Viti Maalumu aliyekuwa akihoji  iwapo Serikali ina taarifa ya kukodishwa kwa kiwanda cha korosho cha Mtama Cashewnut Factory kilichopo katika Jimbo la Mtama kilichokuwa chini ya bodi ya korosho.

 

"Je Serikali inachukua hatua gani juu ya mazingira magumu ya wafanyakazi ambao hawana mikataba ya kazi katika kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na wageni," amehoji Chande

 

Manyanya amesema kiwanda cha kubangua korosho cha Mtama kilibinafsishwa kwa kuuza hisa asilimia 100 kwa Kampuni ya Lindi Farmers Association (LFA) ambayo ndiyo inamiliki.

Hata hivyo, amesema kufuatia umiliki huo, kiwanda hicho kilikodishwa kwa makubaliano maalumu kwa Kampuni ya Sunshine ili iweze kukiendeleza.