Wakazi wa Nkasi wawakataa ndugu wanaotoka Congo

Muktasari:

  • Wakazi hao wanaoishi kata za Kirando, Kabwe na Wampembe, wamekumbwa na hofu kwa kuwa raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hufika maeneo hayo wakileta au kuchukua biashara.

Sumbawanga. Wakazi wanaoishi mpakani Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, wameonyesha hofu kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa ebola.

Wakazi hao wanaoishi kata za Kirando, Kabwe na Wampembe, wamekumbwa na hofu kwa kuwa raia kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hufika maeneo hayo wakileta au kuchukua biashara.

Mkazi wa Wampembe, Abdallah Seif alisema alikuwa na utaratibu wa kuwapokea ndugu, jamaa na marafiki kutoka Congo nyumbani kwake, lakini tangu kuripotiwa ugonjwa huo ameacha.

“Binafsi nimechukua tahadhari ya namna hiyo, kwa kuwa sina utaalamu wa kumbaini mwenye maambukizi ya maradhi hayo,” alisema Seif.

Naye mkazi wa Kabwe, Peter Malema alisema elimu inahitajika haraka ili wananchi wa maeneo ya mwambao wa Ziwa Tanganyika wachukue tahadhari kwa kuwa kuna mwingiliano mkubwa na wageni kutoka Congo.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu alisema wanashirikiana na Wizara ya Afya kuhakikisha ugonjwa huo unadhibitiwa hasa maeneo ya mipakani.

Dk Kasululu amesema wizara imetoa vifaa vitakavyopelekwa katika vituo vya afya na zahanati ili kuwakinga wataalamu wa afya wanapomhudumia mgonjwa wa ebola.