Maxcom sasa kuuza tiketi za Precision Air

Muktasari:

Mkataba huo wa miaka mitatu umesainiwa leo jijini Dar es Salaam

Dar es Salaam. Shirika la Ndege la Precission Air limeingia ubia wa malipo na Kampuni Maxcom Africa utakaowawezesha wateja wake kulipia tiketi zao kwa mawakala wa kampuni hio waliopo maeneo tofauti ndani na nje ya nchi.


Mkataba huo wa miaka mitatu umeingiwa rasmi leo Mei 24, 2018 ambapo mkurugenzi wa Precision  Air, Sauda Rajab na mkurugenzi wa Maxmalipo, Charles Natai wameziwakilisha kampuni zao.


Baada ya kusaini mkataba huo, Natai amesema tangu sasa wateja wa shirika hilo watafanya malipo ya tiketi zao kwa zaidi ya 1,600 kwa mawakala wa Maxcom waliopo nchini, kupitia simu zao za mikononi na tovuti ya kampuni na kupewa namba ya kumbukumbu ya malipo.


"Wateja wote nchini na wale wa Rwanda, Uganda, Burundi na Zambia, watapata urahisi wa kulipia tiketi zao kutokana na upana wa mtandao wetu hivyo tutaongeza wigo wa huduma za Precision," amesema Natai.


Kwa upande wake, Rajab amesema mkataba huo wameufuatilia kwa muda mrefu na wanaamini utaongeza biashara katika shirika lao kutokana na urahisi wa huduma hiyo kwa abiria.


"Nia na lengo la shirika letu bado halijabadilika, tunatamani kuwafikia wasafiri wengi zaidi ndani na nje ya nchi. Malipo kupitia maxmalipo yanaleta urahisi zaidi wa kufikia malengo hayo," amesema Rajab.