TRA yateketeza bidhaa feki za Sh23 milioni

Muktasari:

Bidhaa hizo ziliingizwa nchini kupitia mipaka ya Holili na Tarakea

Moshi. Mamlaka ya Mapato  Tanzania (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro imeteketeza bidhaa mbalimbali za thamani ya Sh23 milioni zilizoingizwa nchini kwa magendo katika  mipaka ya Holili na Tarakea.

 

Akizungumza leo Alhamisi Mei 24, 2018 meneja msaidizi kitengo cha ushuru wa forodha,  Godfrey Kitundu amezitaja bidhaa hizo zilizoteketezwa leo kuwa ni chumvi, vipodozi, mafuta  kula, pipi, vifungashio na vifaa vya hospitali.

 

Amesema TRA husimamia mapato pamoja na kudhibiti biashara za magendo na zile zisizokuwa na viwango.

Amebainisha kuwa mbali na kuteketeza bidhaa  hizo,  pia vyombo vya usafiri vilivyotumika kusafirisha bidhaa hizo vimetaifishwa.

 

Mkaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Edward Mwamilawa amesema  bidhaa zilizoteketezwa zipo ambazo hazina viwango kwa matumizi na ambazo hazitakiwi nchini.