Wabunge waitaka Serikali kuiangalia Tanesco kifedha

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini imeitaka Serikali kuliwezesha kifedha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ili liweze kujiendesha kwa faida.

Wakati kamati ikieleza hayo na kubainisha kasoro zinazojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), wabunge wengi waliozungumza katika mjadala wa bajeti ya Nishati mwaka 2018/19 iliyowasilishwa jana bungeni mjini Dodoma, waligusia utendaji wa shirika hilo, jinsi linavyoshindwa kujiendesha na kukabiliwa na madeni.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, mwenyekiti wake Dustan Kitandula alisema ili Tanesco iweze kumudu kutekeleza majukumu yake, Serikali inapaswa kutoa fedha za kutosha.

Alisema hadi kufikia Februari 2018, wazabuni mbalimbali walikuwa wanaidai Tanesco Sh969 bilioni hivyo kuishauri Serikali kuja na mkakati wa kulipa madeni ya taasisi zake, yakiwamo ya Tanesco.

Mwenyekiti huyo alisema upatikanaji wa umeme nchini bado ni changamoto kutokana na miundombinu mibovu hali inayosababisha kukwama kwa shughuli nyingi za uzalishaji hasa viwandani.

“Kamati inaishauri Serikali kutoa fedha za kutosha kukarabati miundombinu ya umeme ili kupunguza adha kwa wananchi na kuondokana na tatizo la umeme kukatika mara kwa mara,” alisema.

Kuhusu miradi ya Rea, alisema bado inakabiliwa na changamoto katika maeneo mengi, huku vijiji na vitongoji vikirukwa na viongozi na wananchi kutoshirikishwa vya kutosha katika uainishaji wa maeneo. Alisema kamati imebaini ucheleweshwaji wa malipo ya makandarasi wanaotekeleza miradi ya wakala huyo.

Kitandula ambaye pia ni mbunge wa Mkinga (CCM) alisema licha ya makandarasi kuwasilisha maombi ya malipo ya awali tangu Agosti mwaka jana, ulipaji wa madai hayo ulichukua takribani miezi minne kwa baadhi yao na wengine hadi Machi, 2018 malipo yao yalikuwa bado hayajaidhinishwa.

Alisema ucheleweshaji wa malipo utasababishia kuongezeka kwa gharama ya utekelezaji wa miradi pamoja na kutotimia kwa lengo la kuvifikishia umeme vijiji vyote nchini kabla ya mwaka 2020 na kuitaka Serikali kubuni utaratibu mzuri wa ulipaji.

Alisema utekelezaji wa Rea awamu ya tatu unapaswa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi pamoja na viongozi wa maeneno wanaohusika.

Wakichangia mjadala wa bajeti hiyo, mbunge wa Magomeni (CCM), Jamal Kassim alisema madeni ambayo Tanesco inaidai Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), hayatalipika kwa sababu bei ya nishati hiyo haiendani na gharama halisi.

Alisema gharama ya kufikisha umeme Zanzibar haiwiani na bei inayotozwa katika nishati hiyo.

“Si sawa madeni haya hayatokaa kulipika. Ipo haja ya kufanya mabadiliko makubwa katika shirika hilo ili kuongeza ufanisi katika utendaji wake,” alisema.

Mbunge wa Mtwara Mjini (CUF), Maftaha Nachuma alilalamikia nguzo za umeme kutozwa bei ya juu tofauti na uhalisia na kumwomba Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani kuchukua hatua kwa baadhi ya wahandisi.

Mbunge Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya alisema awali Tanesco ilikuwa ikipata hasara ya Sh124bilioni lakini hasara hiyo imeongezeka na kufikia Sh346bilioni. Alisema hasara hiyo inatokana na upugufu wa maji na gharama za uendeshaji. “Tanesco ina madeni ambayo yamepanda kwa asilimia 23. Kabda ya Serikali hii kuingia madarakani ilikuwa na madeni ya Sh738 bilioni ila baada ya kuingia yamefikia Sh958 bilioni na haya si maneno yangu, Ripoti ya CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali), imeeleza,” alisema.