Dhahabu yaigonganisha mikoa ya Geita, Mwanza

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella

Mwanza. Mvutano wa kimasilahi umeibuka baina ya mikoa ya Geita na Mwanza. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel kupiga marufuku usafirishwaji wa madini ghafi (cabon) kutoka mkoani huo kwenda jijini Mwanza.

Wakati huohuo, mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema biashara na masuala ya kiuchumi hayawezi kuwekewa mipaka ya kimkoa, bali kinachotakiwa shughuli hizo kuzingatia sheria na kanuni ikiwemo malipo ya ushuru na kodi.

Kwa upande wake, Gabriel amepiga marufuku uchenjuaji wa madini nje ya Mkoa wa Geita akieleza kuwa nia yake ni kubakiza fursa za ajira mkoani humo na utajiri kuunufaisha mkoa huo.

Mkuu huyo wa mkoa ametangaza Mei 31 kuwa siku ya mwisho kwa cabon yenye madini ya dhahabu kusafirishwa na kuchenjuliwa nje ya Geita, huku wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda vya uchenjuaji wakitakiwa kufungua au kuvihamishia mkoani Geita.

“Pamoja na masuala ya kiuchumi, amri hii pia inalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa wachimbaji na wafanyabiashara ambao hivi sasa wanasafiri umbali mrefu kwenda jijini Mwanza kuchenjua madini yao,” alisema Gabriel akifafanua amri yake.

Wakati mkuu huyo wa mkoa akisisitiza hayo, Mongella amesema biashara na masuala ya kiuchumi hayawezi kuwekewa mipaka ya kimkoa, wilaya, kata wala kijiji, bali kinachotakiwa ni shughuli hizo kuzingatia sheria na kanuni ikiwemo malipo ya ushuru na kodi.

“Maendeleo ya teknolojia na uchumi umefanya dunia kuwa kijiji, hatuwezi kuanza kuwekeana mipaka muhimu ni wahusika kufuata sheria na kulipa kodi na ushuru,” alisema Mongella.

Hata hivyo, mkuu huyo wa mkoa ambaye hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo, alisema anaamini hakuna mgogoro utakaoibuka kati ya Serikali, wafanyabishara na wamiliki wa viwanda vya uchenjuaji kwa sababu lengo kuu la makundi yote ni ujenzi wa uchumi na maendeleo ya wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza jana, makamu mwenyekiti wa Umoja wa Wafanyabiashara na Wamiliki wa Viwanda vya Uchenjuaji wa Dhahabu Mkoa wa Mwanza, George Onyango alisema wamemwandikia barua Mongella kumuomba aingilie suala hilo kwa kuwasiliana na mwenzake wa Geita.

“Badala ya kupiga marufuku usafirishaji wa cabon kutoka Geita kuja Mwanza, Serikali ya Mkoa wa Geita ingeboresha mazingira ikiwemo suala la ulinzi, soko, miundombinu na maeneo ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji wa viwanda vya kuchenjua dhahabu mkoani humo,” alisema Onyango.