VIDEO: Simanzi ilivyotawala miili ya maofisa TIC ikiagwa Dar

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akiwaongoza wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuaga miili ya waliokuwa wafanyakazi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), katika Viwanja vya Karimjee jana. Picha na Venance Nestory

Dar es Salaam. Simanzi ilitawala jana wakati majeneza yenye miili ya maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), waliofariki dunia pamoja walipoagwa na wakazi wa Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee.

Tukio hilo liliibua vilio na simanzi na hata baadhi ya waombolezaji kusikika wakisema, “wamefariki wakiwa bado vijana.”

Maofisa hao waliofariki dunia Jumatatu wiki hii ni meneja wa Tafiti na Miradi, Martin Masalu; kaimu mkurugenzi wa Tafiti, Said Moshi na kaimu mkurugenzi wa Uhusiano, Zacharia Kingu.

Watatu hao walifariki kwa ajali ya gari katika Kijiji cha Msoga, Chalinze mkoani Pwani wakati wakitoka jijini Dar es Salaam kwenda Dodoma kwa safari ya kikazi ambapo gari walilokuwa wakisafiria mali ya Serikali liligonga lori na kusababisha vifo vyao na wengine wawili kujeruhiwa.

Utaratibu wa kuaga

Katika tukio hilo, waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage aliongoza mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuaga miili ya maofisa hao kuanzia saa 5.30 asubuhi na baadaye mazishi ya Kingu yaliyofanyika mchana kwenye makaburi ya Kinondoni.

Mwili wa Masalu ulitarajiwa kusafirishwa jana jioni kwenda Mazimbu mkoani Morogoro ambako utazikwa leo wakati ule wa Moshi utazikwa Monduli mkoani Arusha. Ndugu, jamaa na marafiki walianza kuwasili katika viwanja hivyo kuanzia saa 3.00 asubuhi.

Mbali ya Mwijage pia walikuwepo maofisa wa Serikali, wawekezaji na wadau wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) walioongozwa na mkurugenzi mtendaji, Godfrey Simbeye.

Hata hivyo, tofauti na ilivyozoeleka kwa waombolezaji katika misiba ya Kikristo, hawakupata fursa ya kuiona miili ya wapendwa wao kwa mara ya mwisho kwa kuwa majeneza hayo hayakufunguliwa.

Awali, tangazo lilitolewa likiwaeleza waombolezaji kuwa hawatafunguliwa majeneza hayo kutokana na ushauri uliotolewa na madaktari. Kutokana na tangazo hilo, waombolezaji walitakiwa kupita na kutoa heshima za mwisho mbele ya majeneza, lakini hawakuiona miili ya marehemu.

Umahiri wao watajwa

Akizungumza kabla ya kuaga, Mwijage alisema kituo hicho kimepata pigo kwa kupoteza vijana mahiri kazini.

“Nilipigiwa simu Jumatatu nikiwa Nzega, nilikuwa safarini kutoka Mwanza kwenda Dodoma nikaambiwa hawa vijana wamefariki, nilisikitika sana,” alisema.

Mwijage alisema wamepoteza vijana wachapakazi ambao walifanya kazi hadi usiku ili kuhakikisha kituo hicho kinatekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Tumepoteza wapiganaji waliokuwa tayari kwa mapambano katika utekelezaji wa sera ya ujenzi wa viwanda,” alisema.

Aliwataka wawekezaji kutovunjika moyo kwa kuondokewa na vijana hao akisema kituo kitaendelea kuboresha huduma zake.

Mkurugenzi mtendaji wa TIC, Geoffrey Mwambe alisema amepoteza vijana ambao walikuwa na mchango mkubwa katika kituo hicho.

Alisema wakati wa uhai wao walichapa kazi kwa weledi na uaminifu hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali inavutia wawekezaji kuja nchini.

Mkurugenzi wa TPSF, Simbeye alisema alikuwa akifanya kazi kwa karibu na vijana hao na zilikuwa rahisi kutokana na umariri wa wafanyakazi hao.

“Nimekuwa karibu na vijana hawa kama kiongozi wa sekta binafsi, tulishirikiana, walikuwa wachapakazi,” alisema.

Katibu mtendaji wa Baraza la Biashara Tanzania (TNBC), Raymond Mbilinyi alisema aliwahi kufanya kazi na vijana hao wakati huo akiwa TIC na kwamba, anaukumbuka vizuri mchango wao.

“Hata nilipoondoka nimeendelea kushirikiana nao, tumepata pigo kuwapoteza,” alisema. Wengine waliohudhuria mazishi hayo ni waliowahi kuwa wakurugenzi watendaji wa kituo hicho, Emmanuel Ole Naiko na Clifford Tandali ambaye sasa ni katibu tawala wa Mkoa wa Morogoro.

Mazishi ya Kingu

Mazishi ya Kingu yalifanyika jana kuanzia saa 7.30 mchana hadi saa 8.40 mchana katika makaburi ya Kinondoni ambayo yalihudhuriwa pia na Mwijage.

Mazishi hayo yaliongozwa na mwinjilisti Ernest Huruma wa KKKT Usharika wa Ununio aliyesema katika mahubiri yake kuwa, “maisha ni mafupi, binadamu tuishi tukijua kifo kinaweza kutukuta wakati wowote na mahali popote.”