Trump afuta mkutano wake na Kim, Ofisa Korea Kaskazini aitisha Marekani

Pyongyang, Korea Kaskazini. Muda mfupi baada ya ofisa mwenye ushawishi mkubwa katika Serikali ya Korea Kaskazini kuiambia Marekani kuwa huenda mazungumzo yanayotarajiwa baina ya Rais Donald Trump wa Marekani na kiongozi wa Taifa hilo, Kim Jong-un yasifanyike, Trump amefuta mkutano huo.

Juzi, ofisa huyo, Choe Son-hui ambaye ni miongoni mwa vigogo wa Taifa hilo waliowahi kuliwakilisha miaka ya nyuma katika mazungumzo mbalimbali juu ya mustakabali wa silaha zake za nyuklia, alisema iwapo mazungumzo yatashindikana Marekani ndiyo ya kulaumiwa.

Choe alikaririwa juzi na shirika la habari la nchi hiyo, KCNA akisema kuwa nchi yake haibembelezi mazungumzo na Marekani, bali Wamarekani na washirika wao ndio wanaoipigia magoti kutaka kuzungumza nao.

Kauli ya ofisa huyo ambaye mara nyingi hutoa matamko ya Serikali imekuja wakati ambapo mshauri wa masuala ya ulinzi wa Marekani, John Bolton akiikasirisha Korea Kaskazini wiki iliyopita kwa kusema kuwa watatumia mbinu walizotumia kumng’oa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, ili kuondoa zana za nyuklia.

Vilevile, Korea Kaskazini imekerwa na kauli ya makamu wa rais wa Marekani, Mike Pence aliyoitoa akidai kuwa mazungumzo baina Trump na Kim sio kipaumbele chao na kwamba, wako tayari kutumia mbinu mbadala ili lengo lao litimie.

Pia, Taifa hilo limechukizwa na msimamo wa Rais Trump aliyesema hivi karibuni kuwa hana uhakika kama atakutana na Kim ilhali mipango ya mkutano wao utakaofanyika Juni 12 ikiendelea.

Kufuatia maneno yaliyoikerehesha nchi hiyo, Choe ameamua kuigeukia Marekani na moja kwa moja akarusha kombora kwa makamu wa rais wa Taifa hilo, Pence akimuita kuwa mtu mjinga.

Pia alisema kuwa iwapo Marekani na washirika wake wataendelea kufanya maonyesho ya silaha na vifaa vya kijeshi katika Ghuba ya Korea, nchi yake iko tayari kuonyeshana ubabe na kwamba, hilo wanalisubiri kwa hamu kama mazungumzo ya viongozi hao wa juu yatashindikana.

Choe alisema nchi yake haitaweza kuibembeleza Marekani kukaa nayo mezani kwa kuwa huo haukuwa mpango wao na wala hawajawahi kufikiria kukutana nao kwa ajili ya mazungumzo, isipokuwa jirani yao, Korea Kusini ndiye muhimu zaidi.

Katika siku za hivi karibuni pande hizo mbili zimeonya kuwa mkutano wa Juni 12 unaweza kuahirishwa au kufutwa kabisa, iwapo maneno ya kukatishana tamaa yataendelea.

Msimamo wa Trump

Katika barua aliyomtumia Kim jana, Trump alisema kuwa amefikia uamuzi wa kutokutana naye kutokana na na “hasira kubwa na uadui ulio wazi” vilivyosababishwa na taarifa za hivi karibuni kutoka Korea Kaskazini.

Alisema itakuwa jambo la kushangaza kama atasisitiza mkutano huo ufanyike ilhali kuna hali ya kurushwa kwa maneno kutoka upande wa Korea Kaskazini.

Hata hivyo, katika barua hiyo kwa Kim, Trump alisema wawili hao wanastahili kukutana “siku fulani” ambayo hata hivyo hakuitaja.

“Nilikuwa na hamu kubwa ya kukutana na wewe. Kwa masikitiko makubwa kulingana na kauli za uadui wa wazi zilizoonyeshwa kwenye taarifa yako ya hivi karibuni, naona haitapendeza kufanya mkutano wetu ulioupangwa kwa muda mrefu,” alisema Trump.

“Umekuwa ukisema juu ya uwezo wako wa kinyuklia, lakini wetu ni mkubwa sana na wenye nguvu ambayo ninaomba kwa Mungu haitatakiwi kutumika,” aliongeza.

Jumanne wiki hii, Rais Trump alisema Korea Kaskazini inapaswa kutimiza masharti ili mkutano huo uweze kufanyika na miongoni mwayo ni kuachana na mpango wake wa silaha za hizo.