NMB yapunguza riba, kununua mikopo HESLB

Muktasari:

Sasa kununua mikopo ya waliokopa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB)

Dar es Salaam. Benki ya NMB imetangaza kupunguza riba ya mikopo baada ya kuombwa na wateja wake, kuingia ubia na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa ajili ya kununua mikopo ya wanaokatwa fedha na bodi hiyo.

Akizungumza leo Ijumaa Mei 25, 2018 Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Ineke Bussemaker amesema mbali na kununua mikopo ya wateja watapunguza riba ya mikopo kwa wafanyakazi, wajasiriamali wadogo, wakubwa na wa kati sanjari na kuongeza muda wa marejesho kutoka miezi 60 hadi 72.

“"Wateja wamekuwa wakiomba maboresho katika huduma zetu ikiwemo mikopo, tunataka wateja wetu kupata suluhisho la masuala ya fedha na mitaji kuweza kufanya shughuli zao,” amesema.

“Kwa wafanyakazi sasa riba ya mikopo imepunguzwa kutoka asilimia 19 hadi 17, wajasiriamali kutoka asilimia 21 hadi 19 na wajasirimali wadogo kutoka asilimia 23 hadi 21.”

Kuhusu kununua mikopo HESLB, amesema lengo ni kuunga mkono juhudi za Serikali inayohimiza urejeshwaji wa mikopo hiyo ili kutoa fursa kwa wengine kukopeshwa.

Maboresho mengine yaliyofanywa katika utoaji wa mikopo ni kuruhusu mfanyakazi kupata mkopo ndani ya saa 24, kumuwezesha kuongeza kiwango cha mkopo wakati wowote.

Pia, kumuwezesha kukopa hadi kipindi cha kustaafu huku kiwango cha mkopo kikitajwa kuwa Sh200,000 hadi Sh150 millioni kulingana na uwezo wa mtu kurejesha.

Kaimu mkurugenzi msaidizi wa urejeshaji mikopo wa HESLB, Phidelis Joseph amesema wazo la NMB ni zuri kwa maelezo kuwa linaondoa malalamiko kwa wafanyakazi wanaodai kuelemewa na mikopo ya taasisi tofauti.