Mwanafunzi Saut ajinyonga chumbani

Muktasari:

Taarifa za awali zinadai chanzo ni Liverpool kufungwa.

Mbeya. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu St. Augustin (Saut) tawi la Mbeya, Moses Mashaka amekutwa amekufa ikidaiwa amejinyonga chumbani kwake Mei 27, 2018 kwa kutumia shuka.

Mwanafunzi huyo alikuwa anasoma mwaka wa pili kitivo cha elimu na alikuwa akiishi eneo la Forest ya Zamani jijini Mbeya jirani na chuo hicho.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mussa Taibu, amethibitisha tukio hilo akibainisha taarifa za mwanafunzi huyo walizipata kutoka kwa mmiliki wa nyumba aliyempangisha chumba hicho.

Amesema wanaendelea kuchunguza chanzo chanzo cha tukio lakini taarifa za awali zinadai mwanafunzi huyo amejinyonga baada ya timu yake ya Liverpool kufungwa na Real Madrid katika fainali iliyochezwa jana Mei 27, 2018.

"Kwa taarifa tunazosikia tu lakini hatuna ushahidi ni kwamba kijana huyu jana alibeti akiipa nafasi ya ushindi timu yake ya Liverpool," amesema Kamanda Taibu.

Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo hicho, Bahati Mahimbo amesema, “Taarifa za kifo cha mwanafunzi mwenzetu nimezipata leo mchana kutoka kwa rafiki zake wa karibu ambao walikuwa na ratiba ya kwenda kupata kipaimara katika Kanisa Katoliki, Parokia ya Ruanda jijini hapa."

Amesema walikubaliana na rafiki zake kukutana kanisani lakini hadi muda wa kuanza misa hakuwa amefika na walipouliza ndipo wakapewa taarifa kuwa amejinyonga.