VIDEO: Moto wateketeza jengo Kariakoo

Muktasari:

Moto huo umeanza leo Juni 13 saa 4 asubuhi

Dar es Salaam. Jengo la ghorofa mbili lililopo mtaa wa Agrey na Livingstone, Kariakoo limeteketea kwa moto.

Moto huo umeanza leo Juni 13 saa 4 asubuhi na kuteketeza mali zote zilizohifadhiwa kwenye jengo hilo.

Akizungumza na MCL Digital leo Mwenyekiti wa Wafanyabiashara mtaa wa Agrey Deogratius Sanya amesema moto ulianza kidogokidogo kwenye moja ya stoo iliyokuwa juu baada ya kutokea shoti ya umeme na baadae moto huo ukasambaa.

Amesema baada ya saa mbili Jeshi la Zimamoto na uokoaji walifika na magari  yenye maji lakini hayakuwa na uwezo wa kuuzima.

" Magari yalifika lakini hayakuwa na uwezo wa kurusha maji lakini baada ya muda ilifika kampuni binafsi iliyoshirikiana na kikosi cha bandari"amesema Sanya.

Ameongeza kuwa kikosi cha bandari kiliweza kuudhibiti moto huo  usisambaye na kuleta madhara zaidi.

Msemaji wa kikosi cha zimamoto na uokoaji Joseph Mwasabeja amesema kikosi cha zimamoto na uokoaji kilifika na kukuta moto umesambaa kwenye jengo zima lakini kutokana na jengo hilo kuwa nauzio maji yalishindwa kupenya kwa urahisi.

"Tumefika na kukuta moto umesambaa tulichofanya nikuanza kubomoa kingo zilizowekwa  kuzunguka jengo ili kuwezesha maji kupenya kirahisi" amesema Mwasabeja.