Ushuru wa maji juu kwa asilimia 60

Wabunge wakiwa ndani ya Ukumbi wa Bunge wakimsikiliza Waziri wa Fedha na Mipango alipokuwa akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Serikali itaanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 

Dodoma. Serikali imeongeza ushuru wa forodha kwa maji (mineral water) kwa asilimia 60 badala ya asilimia 25 ya awali.

 Hayo yameelezwa leo, Juni 14 na Waziri wa Fedha na Mpango, Dk Philip Mpango wakati akiwasilisha bajeti kuu kwa mwaka wa fedha 2018/19.

“Hatua hii ni muhimu katika kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya nchini vinavyozalisha bidhaa hiyo,” amesema

Pia, serikali itaanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwenye soseji  kwa mwaka mmoja.

“Lengo la hatua hii ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya uchakataji wa nyama nchini, hivyo kuongeza thamani yake,” amesema.

 Mafuta

Kadhalika, itaanza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 35 badala ya asilimia 25 kwa mwaka mmoja kwenye mafuta ya kula yaliyochakatwa kwa kiwaango cha kati na cha mwisho (semi-refined, refined/double refined oil).

Kwa mfano alizeti, mawese, soya, mzaituni, nazi, karanga, na mahindi.

“Ongezeko hilo la ushuru wa forodha linatarajiwa kulinda uzalishaji wa mafuta ya kula na kuhamasisha uchakataji wa mbegu za mafuta zinazozalishwa nchini badala ya kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi,” amesema

Amesema hatua hii inatarajiwa kupunguza fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

 Viberiti

Pia imependekeza kutoza ushuru wa forodha wa asilimia 25 au kwa kilo moja ya viberiti (safety matches) vinavyotambuliwa kwa kutegemea kiwango kipi ni kikubwa.

“Hatua hii inazingatia kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zina uwezo wa kuzalisha viberiti na kutosheleza mahitaji katika soko, hivyo kuwepo na umuhimu wa kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hiyo,”amesema