Umaskini, ukosefu wa ajira vikwazo vya bajeti

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango


Muktasari:

Tanzania bado ina kiwango kikubwa cha umaskini ingawa kuna matarajio ya kuendelea kupungua.

Dar es Salaam. Kiwango kikubwa cha umaskini, ukosefu wa fursa za ajira na wigo mdogo wa ukusanyaji mapato ya ndani ni miongoni mwa mambo ambayo Serikali imeyazingatia katika kuandaa bajeti iliyowasilishwa bungeni jana kwa kuwa ni changamoto kuu za Taifa.

Akiwasilisha bajeti hiyo ya maneno 14,602 bungeni jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema pamoja na hayo, pia wamezingatia umuhimu wa sekta ya kilimo inayoajiri Watanzania wengi pamoja na mahitaji makubwa ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii hasa maji, afya na elimu bora.

Alisema maeneo hayo yamezingatiwa kwa kuangalia fursa zilizopo kuwa ndio changamoto kuu za kiuchumi na kijamii zinazolikabili Taifa.

Akifafanua, alisema Tanzania bado ina kiwango kikubwa cha umaskini ingawa kuna matarajio ya kuendelea kupungua.

Akinukuu takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dk Mpango alisema kiwango cha umaskini kimepungua kidogo kutoka asilimia 28.2 (2011/12) hadi asilimia 26.4 (2015/16).

“Matarajio ni kuwa utafiti wa matumizi ya kaya unaoendelea hivi sasa utatupatia taarifa nzuri zaidi ya kuendelea kupungua,” alisema.

Ukosefu wa ajira

Kuhusu fursa za ajira, waziri huyo alisema takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 10.4 ya Watanzania hawana ajira na kuwa kati ya vijana 800,000 wanaohitimu masomo yao kila mwaka, Serikali ina uwezo wa kuajiri wastani wa watu 40,000.

Kwa takwimu hizo, kila mwaka wanaingia mitaani vijana 760,000 wanaoajiriwa na sekta binafsi, ajira zisizo rasmi na wengine kukosa ajira.

Akizungumzia kilimo, Dk Mpango alisema pamoja na kuajiri asilimia 66 ya Watanzania na kuchangia asilimia 30 ya Pato la Taifa, kwa miaka 10 kimeendelea kukua kwa kasi ndogo ya wastani wa asilimia 3.7 kwa mwaka.

Alisema hali hiyo inatokana na uwekezaji mdogo, tija ndogo, utegemezi wa mvua na mchango mdogo wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa wa asilimia 5.5.

Vilevile alisema licha ya mahitaji makubwa ya upatikanaji wa huduma muhimu za jamii, hali ya miundombinu ya umeme, usafiri na usafirishaji bado havikidhi mahitaji ya uchumi kukua kwa kasi.

“Mathalan, mtandao wa barabara nchini ni kilomita 86,472 lakini kati yake, asilimia 9.7 tu ndiyo za kiwango cha lami,” alisema.

Pamoja na juhudi za kuwekeza kwenye umeme, Dk Mpango alisema mahitaji ya umeme wa majumbani na viwandani bado ni makubwa ikilinganishwa na uwezo wa uzalishaji wa nishati hiyo.

“Mitambo iliyopo kwa sasa ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,424.6 ikilinganishwa na mahitaji ya zaidi ya megawati 3,000 ili kuhimili mahitaji ya uchumi wa viwanda,” alisema waziri huyo.

Pia alizungumzia wigo mdogo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, akisema uwiano wake na Pato la Taifa ni asilimia 15 ikilinganishwa na wastani wa asilimia 17 kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara.

Bajeti hiyo pia imezingatia fursa zilizopo, hususan nguvukazi ya vijana, rasilimali na fursa katika kilimo, madini, gesi, vivutio vya utalii, viwanda vya huduma za kilimo, vyanzo vya uzalishaji wa umeme, biashara na huduma za usafirishaji wa mizigo kwenda nchi jirani.

Tathmini ya bajeti iliyopita

Waziri Mpango alisema katika kipindi cha Julai 2017 hadi Aprili 2018 mapato kutoka vyanzo vyote yalifikia Sh21.89 trilioni sawa na asilimia 69 ya lengo la kukusanya Sh31.71 trilioni.

Katika mchanganuo, mapato ya ndani yakijumuisha ya halmashauri yalifikia Sh14.84 trilioni ikilinganishwa na lengo la kukusanya Sh19.98 trilioni (asilimia 74.3).

Kati ya kiasi hicho, makusanyo ya kodi yalikuwa Sh12.61 trilioni, yasiyo ya kodi ni Sh1.79 trilioni na ya halmashauri yalifika Sh437.6 bilioni.