Wadau wajadili changamoto, utatuzi maombi ya mikopo elimu ya juu

Meneja wa Habari, Elimu na Mawasiliano, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Omega Ngole

Dar es Salaam. Uhakiki wa vyeti, ujazaji wa fomu kwa njia ya mtandao vimeelezwa kuwa changamoto kubwa inayowakabili wanafunzi wanaoomba mikopo katika Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).

Changamoto nyingine ni wanafunzi hao kupeleka vyeti visivyosomeka, vingine vikiwa vimeambatanishwa na picha zilizopigwa kwa kutumia simu zikiwa na vipicha vya katuni (emoji).

Akizungumza jana katika mkutano wa wadau wa HESLB, Mkurugenzi wa Tehama wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Cuthbert Simalenga alisema kuna waombaji ambao wamekuwa wakifanya udanganyifu katika malipo. “Kuna malipo ya Sh3,000 kwa ajili ya uhakiki wa vyeti ambapo wanafunzi hutakiwa kuwasilisha risiti baadhi yao huleta zisizo halali,” alisema.

Alisema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakipeleka nyaraka zisizosomeka ikiwamo kufutika kwa namba ya ingizo (entry number) hivyo kuifanya kazi ya uhakiki kuwa ngumu.

Alisema wanafunzi wengi hawafuati utaratibu ulioelekezwa wa kufungua akaunti binafsi katika tovuti ya uhakiki na badala yake wanakabidhi jukumu hilo kwa watoa huduma wa vibanda vya mtandao, hivyo kushindwa kupata majibu yao.

“Kuna wanafunzi wametuma vyeti vya shule vilivyotolewa na mamlaka nyingine ikiwamo za Zanzibar,” alisema.

Hata hivyo, ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata fursa ya kutuma maombi na kupata majibu kwa wakati, Rita imeongeza idadi ya wafanyakazi kutoka 18 hadi 28.

“Awali, tulikuwa tunafanya kazi hadi saa 12 jioni lakini kuanzia Mei 9, tumeongeza muda na tunafanya kazi hadi saa 2:00 usiku ili kuhudumia maombi mengi kwa muda mfupi na tumefikia kuhakiki vyeti 3,000 kwa siku kutoka 2,500,” alisema Simalenga.

Mmbali ya changamoto hizo, mkuu wa idara wa uendeshaji mitihani wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Edgar Kasuga alitaja nyingine ya utapeli akisema kuna watu wanaowatoza wanafunzi kati ya Sh20,000 na 30,000 za kufanya uhakiki wa vyeti vya kitaaluma ili kukamilisha mchakato wa uombaji wa mikopo.

“Vyeti vya kitaaluma kama cheti cha ualimu, cheti cha kumaliza kidato cha nne na cha sita havihakikiwi ili kukamilisha mchakato wa kuomba mkopo wa elimu ya juu,” alisema.

Mkurugenzi Mkuu wa HESLB, Abdul -Razaq Badru alisema hadi kufikia jana, wanafunzi 18,820 walikuwa wameshakamilisha maombi yao, huku wanafunzi 52 wakifungua akaunti kwenye mtandao wa kuomba mikopo.

Aliwataka wanafunzi waombaji wakumbuke kuwa kuna muda maalumu wa kuomba.

“Tunaomba na ninasisitiza wanafunzi someni maelekezo yote yaliyowekwa kwenye fomu, kwa sababu imebainika baadhi yenu mnajaza nusu. Ukifanya kitu tofauti na maelekezo yaliyowekwa unakosa sifa ya kupata mkopo hata kama unastahili,” alisema Badru.

Pia aliwataka wanafunzi walisomeshwa kwa ufadhili katika shule za awali, kuhakikisha wanaweka nyaraka zilizo sahihi zitakazotambulisha hilo wanapokuwa wakituma maombi yao ya mikopo.