Mtanzania anayefanya kazi Boeing

George Jonas

Muktasari:

  • Mtanzania huyo juzi alipewa fursa ya kuzungumza wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mtanzania anayefanya kazi katika kampuni ya Boeing ameelezea jinsi safari yake ya maisha ilivyokuwa mpaka kutua katika kampuni kubwa ya ndege duniani.

Mtanzania huyo juzi alipewa fursa ya kuzungumza wakati wa mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 787-8 Dreamliner katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Anafanya kazi katika makao makuu ya kampuni hiyo huko Seattle, Washington akiwa mhandisi wa umeme mwenye jukumu la kuangalia usalama wa mifumo ya ndege na kuhakikisha kwamba inafanya kazi kwa uhakika.

Jana, mhandisi huyo, George Jonas alitembelea ofisi ndogo za Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), zilizopo Mtaa wa Samora jijini hapa na kusimulia kwa undani safari iliyomfikisha katika shirika hilo kubwa la ndege duniani.

Kabla ya kujiunga na Boeing, Jonas ambaye elimu yake ya msingi mpaka sekondari alisoma katika shule za Serikali za Ubungo NHC, Azania na Ilboru, alianza kufanya kazi katika kampuni ya Bombadier mwaka 2006/7 akiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Wichita State kilichopo Kansas, Marekani ambako pia alisema kuna tawi la kampuni hiyo ya ndege yenye makao yake makuu huko Montreal, Canada.

Alijiunga na kampuni hiyo akiwa katika mafunzo kwa vitendo, lakini baadaye aliajiriwa.

Jonas anasimulia kuwa mwaka 2011 aliona nafasi ya kazi katika kampuni ya Boeing kwenye mitandao na kuamua kuomba nafasi hiyo. Alisema aliitwa kwenye usaili na kufanikiwa kuchaguliwa.

“Nakumbuka kipindi kile kulikuwa na mdororo wa kiuchumi, hali ilikuwa mbaya sana Marekani. Kampuni zilikuwa zinapunguza watu, kampuni yetu nayo ilitangaza kupunguza watu mpaka asilimia 50. Hata hivyo, bosi wangu alinihakikishia kwamba wamewekeza kwangu, hivyo mimi sitaondoka.

“Nilienda kufanya usaili nikiwa sina wasiwasi kwa sababu tayari nilikuwa nina kazi. Basi, siku moja nikapigiwa simu nikaambiwa nimepita kwenye usaili, nikafurahi sana, lakini ugumu ukawa ni kumweleza yule bosi wangu wa Bombardier, maana alinisaidia sana. Huwezi kuamini, aliniruhusu kwenda Boeing,” alisema Jonas.

Alisema miaka saba ambayo amefanya kazi katika kampuni ya Boeing na mingine mitano akiwa Bombadier, amejifunza mambo mengi yanayohusiana na uhandisi wa umeme katika ndege.

Hajasahau nyumbani

Jonas alisema kwa hapa nchini anaendesha mradi wa Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hesabu, (STEM – Science, Technology, Engineering, Mathematics) ambao unalenga kuhamasisha wanafunzi wa shule za msingi kupenda masomo ya sayansi.

Alisema alijua kwamba Serikali inanunua ndege, hivyo aliona ni wakati mwafaka kuchukua likizo na kurudi nchini wakati wa ujio wake ili pamoja na mambo mengine kuhamasisha wanafunzi wa shule ya msingi aliyosoma ya Ubungo NHC.

“Huo ni utamaduni ambao upo pale Boeing na wanani-support katika initiative yangu hii. Watu wanaweza kujiuliza kwa nini nilichagua kwenda shule yangu ya msingi na siyo sekondari, sababu ni kwamba nina connection na ile shule,” alisema.

Alisema anaamini kwamba mtoto yeyote anaweza akafanya jambo lolote akijengewa uwezo. Hivyo alisema ameamua kuhamasisha watoto kupitia mpango wa STEM kusoma masomo hayo ili kujua namna ndege inavyotengenezwa.

Katika mpango huo, alisema ameungwa mkono na mamlaka za Serikali ambazo zimeona kwamba hilo ni jambo zuri na kila sehemu aliyopita kuomba kibali cha kwenda na wanafunzi kupokea ndege, alipata ushirikiano ikiwamo Ofisi ya Rais, Tamisemi na Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

“Shughuli ninazozifanya zinalenga kutoa hamasa kwa wana-funzi kusoma masomo ya STEM. Nimekuja na vifaa vinavyoonyesha jinsi wanavyo-hack computer ili kufundisha wanafunzi,” alisema Jonas.

Mwalimu Mkuu ampongeza

Awali, mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Ubungo NHC, Miriam Marwa alimpongeza Jonas kwa kuamua kuikumbuka shule aliyosoma kwa sababu watu wengi wenye mafanikio hawafanyi hivyo.

Alisema mpango wa Jonas wa kuhamasisha masomo ya sayansi utawasaidia wanafunzi wengi kuhamasika kusoma masomo hayo.

Alisema shule hiyo inampa nafasi ya kukutana na wanafunzi na kuzungumza nao.

“Wiki iliyopita alikutana na baadhi ya wanafunzi wetu na wa-kati ndege mpya inawasili nchini aliomba kwenda na wanafunzi kuipokea. Nilifanya kuchagua wanafunzi 19 waliofanya vizuri kwenye mitihani yao kuanzia darasa na nne mpaka la saba,” alisema.