Tuesday, July 10, 2018

Kifo cha mchuuza mbogamboga chazua taharuki, aliaga kwenda kulipa madeniKamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe 

By Burhani Yakub, Mwananchi byakub@mwananchi.co.tz

Tanga. Baadhi ya wakazi jijini Tanga wameingia kiwewe baada ya mchuuzi wa mbogamboga kukutwa ameuawa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe alisema mchuuzi huyo, Hidaya Shaaban (34) aliuawa katika kitongoji cha Japan kilichopo kata ya Tangasisi.

Wakazi wa nyumba aliyokuwa akiishi Hidaya walilieleza gazeti hili kuwa, Jumamosi iliyopita jioni aliwaaga kwamba anakwenda kulipa madeni na tangu siku hiyo hakurejea hadi juzi walipopata taarifa za mwili kuonekana karibu na Sekondari ya Japan na kwamba, walipokwenda wakamtambua.

“Mauaji haya yametushtua, alituaga kwa furaha kwamba anakwenda kulipa madeni, hatukumuona tena hadi tuliposikia ameuawa,” alisema Jumaa Haji.

Kamanda Bukombe alisema mwili wa Hidaya uliburuzwa umbali wa mita 500 kutoka sehemu alipouawa.

Alisema wanasubiri taarifa za uchunguzi kutoka Hospitali ya mkoa ya Bombo Kuhusu mauaji hayo.

Inaelezwa mwili huo ulikuwa na majeraha kichwani na shingoni, huku polisi wakiomba wenye taarifa zinazoweza kusaidia kukamatwa watuhumiwa kusaidia.

-->