Twaweza yasema haihusiki kusambaza barua ya Costech mitandaoni
Muktasari:
Eyakuze amesema barua inayosambaa mitandaoni haina muhuri wa taasisi yao.
Dar es Salaam. Saa chache baada ya Tume ya Sayansi na Teknolojia, (Costech) kusema wamesikitishwa na kitendo cha kusambaa mitandaoni kwa barua waliyowaandikia taasisi ya Twaweza, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Aidan Eyakuze amesema hawajahusika kuisambaza.
Eyakuze ameyasema hayo leo Julai 12, kwenye ukurasa wa twitter wa taasisi hiyo.
“Kama tulivyosema awali, tumepokea barua kutoka Costech na tunaifanyia kazi. Twaweza haijasambaza barua hiyo wala kuhusika kuisambaza kwenye mitandao ya kijamii,” imesema taarifa hiyo
Eyakuze amesema, barua zote zinazopelekwa Twaweza huwekwa muhuri mbele ya aliyetumwa kuipeleka pamoja na risiti.
“Barua inayosambaa mitandaoni haina muhuri wetu, tunaheshimu mawasiliano yote yanayofanywa na wadau wetu,” amesema
Leo asubuhi, Kaimu Mkurugenzi wa Costech Dk Amos Nungu alizungumza na wanahabari na kusema wamesikitishwa na kusambaa mitandaoni kwa barua hiyo waliyopelekewa Twaweza.
Soma Zaidi: