Wasanii wakongwe walivyomzungumzia marehemu John Mhina

John Mhina ‘John Vaga’


Muktasari:

Taarifa za kifo chake zilithibitishwa na mdogo wake Joseph Mhina ‘Joe'

Moja ya taarifa zilizoshtua wiki hii ni pamoja na kifo cha mwanamuziki wa siku nyingi wa Bendi ya Tanzanite, John Mhina ‘John Vaga’ aliyefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Taarifa za kifo chake zilithibitishwa na mdogo wake Joseph Mhina ‘Joe’ ambaye alieleza kuwa kaka’ke alifariki akiwa njiani kupelekwa Hospitali ya Lugalo. “Ni kweli kama mlivyosikia ndugu yetu alifariki Alhamisi alfajiri, na hii ni baada ya hali yake kubadilika akiwa nyumbani kwake Bunju ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Rabininsia iliyopo Tegeta na baada ya madaktari kuona hali yake ni mbaya waliagiza apelekwe hospitali ya Lugalo kwa ajili ya matibabu zaidi.

“Lakini kwa bahati mbaya wakati ndugu wakiwa njiani kumpeleka Lugalo alifariki,” anasema Joe ambaye ni mdogo wa mwisho wa John.

Joe anasema kaka yake huyo kwa muda wa wiki tatu zilizopita hali yake haikuwa nzuri na alikuwa akiendelea na dawa za ugonjwa wa moyo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu, huku akichukuliwa vipimo baada ya kuibuka magonjwa mengine ambayo hakuyaweka wazi. Mwanamuziki huyo ambaye pia anaelezwa kuwahi kupanda jukwaa moja na mwanamuziki maarufu duniani, Michael Jackson, katika moja ya maonyesho yake nchini humo, enzi za uhai wake alipata umaarufu kutokana na kuimba nyimbo za kukopi. Pia akiwa na bendi yake hiyo walitoa vibao mbalimbali kikiwemo kiitwacho Pugu Kariakoo kilichopendwa sana kipindi cha miaka ya 1980.

Wanamuziki walivyoupokea msiba

Akizungumza na Mwananchi, Katibu wa Chama cha Dansi Tanzania (Chamudata), Hassan Msumari anasema Mhina na bendi yao walichangia kuleta mapinduzi katika muziki wa dansi kwa kupiga kisomi na kisasa zaidi ambapo walisafiri nchi mbalimbali kwa mialiko ikiwemo Japan, Marekani, Dubai na nyinginezo.

Msumari anasema kwa safari zao hizo ndipo walipata bahati hadi ya kutumbuiza na Michael Jackson jukwaa moja, mwanamuziki ambaye kila aliye kwenye sanaa ya muziki alitamani kufanya naye kazi.

Kwa hapa nchini anasema walikuwa wakipiga zaidi kwenye hoteli kubwa ikiwemo Whitesands, Kilimanjaro Hyyat na New Afrika ambapo walikuwa na mashabiki wengi.

Baadhi ya wanamuziki ambao amewahi kuwa nao karibu akiwemo King Kikii, anasema John ameacha pigo katika muziki wa dansi ambao ulikuwa bado unahitaji ushauri na uzoefu wake.

King Kikii anaongeza kuwa vijana wana mengi ya kuiga kwa msanii huyo ambaye aliweza kushikana na bendi yake hadi mauti yalipomkuta tofauti na wa sasa ambao hutangatanga katika bendi tofauti.

Naye Ally Zahir Zorro, mmoja wa wasanii wakongwe hapa nchini, anasema atamkubuka Mhina kwa namna alivyokuwa akiheshimu kazi yake na jamii kwa ujumla kwani alikuwa si mtu wa maneno mengi na alikuwa mtulivu pamoja na umaarufu aliokuwa nao.

Mpiga ngoma wa Bendi ya Tanzanite, Peter Bolcha anasema watamkumbuka daima John kutokana na kuwa mwalimu na mshauri mzuri katika bendi yao.