Takukuru yawaonya wakurugenzi kuwalipa makandarasi kabla

mkuu wa Takukuru mkoani Geita, Thobias Ndaro

Muktasari:

  • Mbali na kuwalipa makandarasi kwa kazi ambazo hazijafanyika, Takukuru imebaini makandarasi kulipwa gharama kubwa za kazi walizofanya tofauti na mwongozo wa gharama za BOQ.

Geita. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Geita, imesema baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri huwalipa makandarasi fedha kwa kazi ambazo hazijafanyika ni kinyume na utaratibu.

Mbali na kuwalipa makandarasi kwa kazi ambazo hazijafanyika, Takukuru imebaini makandarasi kulipwa gharama kubwa za kazi walizofanya tofauti na mwongozo wa gharama za BOQ.

Hayo yalisemwa juzi na mkuu wa Takukuru mkoani hapa, Thobias Ndaro wakati akitoa taarifa ya utendaji kwa Julai 2017 hadi Juni 2018.

Ndaro alisema katika ufuatiliaji matumizi ya fedha za miradi ya maendelo, wamebaini makandarasi kufanya kazi za miradi kinyume na mwongozo.

Alisema tayari wamewaagiza makandarasi chini ya usimamizi wa halmashauri kuzirudia kazi zenye upungufu na kuzikamilisha kwa mujibu wa mikataba.

Pia, amewaagiza wakurugenzi ambao halmashauri zao zililipa fedha kwa kazi ambazo hazijafanyika kuhakikisha wakandarasi wanakamilisha kazi zote walizolipwa ndani ya muda wa mkataba.

Ndaro alisema taasisi hiyo imeendelea na uchunguzi wa tuhuma za rushwa kwenye matumizi ya fedha za maendeleo katika miradi mbalimbali yenye thamani ya zaidi ya Sh60 bilioni.

Alisema uchunguzi unafanywa kwenye miradi ya barabara zinazojengwa kwa kiwango cha lami mjini Geita, miradi ya maji inayofadhiliwa na benki ya dunia kutoka Ziwa Victoria katika kijiji cha Chankolongo uliopo wilayani Geita na wa Nyamtukuza uliopo wilayani Nyang’hwale.

Miradi mingine inayochunguzwa ni ufuatiliaji miradi ya chanjo ya surua na Rubella, matumizi ya fedha za mfuko mkuu, madeni ya pembejeo na madai ya mawakala waliosambaza pembejeo mkoani hapa.