‘Mabosi’ kiwanda cha Five Star wafikishwa mahakamani

Muktasari:

Ni kwa kuwafanyisha kazi raia wa kigeni bila vibali vya kazi


Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Uchapishaji cha Five Star,  Ashikabbas Karim(30) maarufu kama Shakirali na  wafanyakazi wake wanne, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu mashtaka tisa, likiwamo la  kuajiri raia wa kigeni ambao hawana vibali  vya kazi.

Mbali na Karim, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ya jinai namba 231 ya mwaka 2018 ni Aroygam Mocharias (38), (mwendeshaji) Mahesh Goud( 32) maarufu kama Budige,(Msimamizi wa Uzalishaji) HarishRaju Poojary(35) maarufu kama Bangeara, (Msimamizi) na Kiran  Kumar(30) maarufu kama Koneti (Fundi) wote raia wa India na wakazi wa Vingunguti, jijini hapa.

 

Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Arnold Peter akisaidiana na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, amedai leo Julai 17, 2018 kuwa  washtakiwa hao walitenda makosa hayo Julai 12, 2018 katika Kiwanda cha Uchapishaji cha Five Star kilichopo eneo la  Vingunguti, Wilaya ya Ilala.

Julai 13 mwaka huu, Naibu Waziri wa Viwanda, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Anthony Mavunde aliagiza kiwanda hicho cha uchapishaji kwa tuhuma za kuwaajiri raia wa kigeni wasio na vibali vya kazi. Mavunde alifanya ziara ya ghafla kiwandani hapo.