Majaliwa ahimiza umoja, mshikamano

Wananchi wa Makunduchi mkoa wa kusini Unguja wakipigana kwa kutumia majani ya mgomba ambapo mapigano hayo ni sehemu ya sherehe za mwaka kogwa.Picha na Muhammed Khamis.

Muktasari:

Majaliwa asisitiza kudumishwa mila na desturi


Zanzibar. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ipo haja ya viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kuhubiri umoja na mshikamo.

Pia, kuzikumbusha jamii kuenzi mila na tamaduni.

Majaliwa amesema hayo alipozungumza na wananchi wa Makunduchi mkoani Kusini Unguja leo Julai 18,2018 katika sherehe za kimila (Kogwa) ambazo hufanyika kila mwaka.

Amesema kuhifadhi mila na desturi huwafanya wananchi kuendelea kuishi katika mazingira bora ya ujirani mwema.

Majaliwa amesema licha ya kuwa Tanzania ina makabila yasiyopungua 120, ni jambo la faraja wananchi wa Makunduchi kudumisha mila walizorithi kwa wazazi wao tangu karne ya 18.

Amewataka wazazi wa eneo hilo kuhakikisha utamaduni huo unaenziwa na kuendelezwa vizazi hadi vizazi.

Waziri mkuu amesema sherehe hizo pia zinakuza utalii kwa kuwa wageni kutoka Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya wamehudhuria.

Mwakilishi wa Makunduchi, Haroun Ali Suleiman amesema anaamini sherehe hizo zitaibua fursa mpya ya ushirikiano.

Naibu waziri wa vijana, utamaduni na michezo, Lulu Msham Abdalla amesema sherehe hizo ni fursa kwa Zanzibar kutangaza utalii.

Amesema pia zitaongeza kipato kwa wajasiriamali.

Naibu waziri amesema wamejipanga kuona sherehe hizo zinaboreshwa.