Mawaziri watembelea mradi wa umeme Rusumo, kukamilika 2020

Muktasari:

Hayo yameelezwa leo Julai 19, 2018 na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alipotembelea mradi huo akiwa na mawaziri wa Burundi na Rwanda

Ngara. Serikali za Tanzania, Burundi na Rwanda zimeridhishwa na hatua ya ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme wa maji katika maporomoko ya mto Rusumo wilayani ya Ngara mkoani Kagera unaotarajia kukamilika Februari, 2020.

 

Hayo yameelezwa leo Julai 19, 2018 na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani alipotembelea mradi huo akiwa na mawaziri wa nchi hizo, kufanya kikao cha ndani.

 

Amesema mradi huo unaojengwa na wakandarasi kutoka China chini ya usimamizi wa nchi tatu, utagharimu dola 468milioni za Marekani, kati ya hizo, dola 340milioni zitatumika kuchimba bwawa na dola 128 milioni  kujenga njia za kusafirisha umeme.

 

Amesema mradi huo utazalisha megawati 80 na kila nchi itapata megawati 27.

 

Kalemani amesema umeme huo utachochea uwekezaji katika sekta ya viwanda ikiwemo uzalishaji wa madini na nickel katika kata ya Bugarama, kuwataka wananchi kuzalisha mazao kwa wingi kwa ajili ya chakula na biashara.

 

"Tunatarajia kupokea hata watalii kutokana na eneo hili kuwa lenye kuvutia likiwa na milima mabonde. Mradi huu pia utakuwa na miundombinu inayochochea kuharakisha maendeleo,” amesema Dk Kalemani.

 

Mbunge wa Ngara (CCM), Alex Gashaza ameiomba Serikali kujenga njia mbadala kusaida wananchi kuvuka mto Ruvubu kwa maelezo kuwa kivuko kilichopo hakitumiki baada ya mto huo kujaa maji.

 

Amesema kwa sasa wananchi wanavuka mto huo kwa kutumia mtumbwi kwa gharama ya Sh4,000 kwenda na kurudi.