Kashikashi wanazopitia wanaume kipindi cha ujauzito wa wenza wao

Inapofikia suala la kuwa na ujauzito salama au kupata mtoto, mara nyingi nguvu kubwa huelekezwa kwa akina mama.

Akina baba watarajiwa hawaonekani kama wana mchango mkubwa katika kipindi chote cha ujauzito.

Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa hapa nchini, ushiriki wa akina baba wakati wa kipindi cha ujauzito na baada ya kujifungua ni mdogo na hauridhishi.

Lakini, ukweli ni kuwa wanaume pia hupitia changamoto katika kipindi cha ujauzito.

Achilia mbali majukumu ambayo wanaume huwa nayo kipindi cha ujauzito, lakini pia hupitia changamoto nyingi za kimwili, kiakili na kisaiokolojia kwa kipindi ambacho wake zao wanakuwa wamebeba ujauzito.

Utafiti uliopewa jina la “Uzoefu wa wanaume wanapopitia mabadiliko katika kipindi cha ujauzito na maisha ya kulea…” uliochapishwa na Shirika la Kimarekani la ‘the US National Library of Medicine’ mwaka 2016, unaonyesha kipindi ambacho mama anakuwa amebeba ujauzito, wanaume wengi hupitia changamoto nyingi ikiwamo msongo wa mawazo.

Mtaalamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Afya Muhimbili, Dk Deus Kitapondya anasema, “Mwanamke anapojifungua, kila kitu kinabadilika ndani ya nyumba, hivyo kuna mambo mengi ambayo mwanaume anatakiwa kuyapitia. Hii inaweza kusababisha msongo wa mawazo au inaweza kumuathiri kisaikolojia.”

Dk Kitapondya anasema katika kipindi hicho, kunakuwa na ongezeko la matumizi ndani ya nyumba.

Anasema hii huendelea hata baada ya mwanamke kujifungua, yote haya yanaweza kumsababishia hali ya msongo wa mawazo mwanaume kama atakuwa hajajiandaa vema.

Hata hivyo, anasema ingawa jitihada nyingi hufanyika kuwahamasisha wanaume kushiriki kikamilifu kwenye kipindi cha ujauzito, tafiti zilizofanyika kwenye nchi za uchumi mdogo na uchumi wa kati zinaonyesha ushiriki wa wanaume bado ni mdogo.

INAENDELEA UK.18

Anasema utafiti uliofanywa wilayani Masasi, Mkoa wa Mtwara uliopatiwa jina la “Mtazamo juu ya ushiriki wa wanaume wakati wa kipindi cha ujauzito na kipindi cha kujifungua.”

Matokeo yake yalibaini wanawake wanapendelea kuongozana na waume zao wanapoenda kliniki hususani katika siku za kwanza baada ya kujigundua kuwa ni wajawazito.

Wakati kwa upande wa wanaume, matokeo ya utafiti yalionyesha hawataki kushirikishwa zaidi wakati wa kipindi cha ujauzito na kipindi cha baada ya kujifungua.

Utafiti huo pia ulibaini jamii kwa ujumla inamtazamo kwamba, wanaume kazi yao pekee ni kutafuta fedha tu katika kipindi hicho kwa ajili ya kuwasaidia wanawake hao na si kufuatilia afya ya mama na hata mtoto baada ya kujifungua.

Uoga wa wanaume kufanya vipimo kama cha Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na pia, miundombinu mibovu ya hospitali ni miongoni mwa sababu ambazo zinachangia kuwazuia wanaume kushiriki kikamilifu wakati wa kipindi cha ujauzito wa wenza wao.

Kutokana na mtazamo huu, Mwananchi lilitembelea wodi ya wajawazito katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, lengo likiwa kujionea namna gani wanaume wenye wake wajawazito wanavyojitokeza kuwasindikiza wenza wao kuhudhuria kliniki hospitalini hapo.

Mwandishi alibaini idadi kubwa ya wajawazito walikuwa wanaenda kliniki peke yao bila kusindikizwa na wanaume zao.

Wengi wao walionekana kuchoka na wengine walilazimika kulala kwenye viti wakati wakisubiri zamu zao za kuonana na daktari.

Japokuwa uchunguzi uliofanyika ulibaini kwamba wanawake wengi walifika hospitalini hapo bila kusindikizwa na wenza wao, Mwananchi lilifanikiwa kufanya mahojiano na baadhi ya akina baba wachache ambao siku hiyo waliongozana na wake zao kuhudhuria kliniki.

Baada ya mahojiano, wengi wao walikuwa na mitazamo tofauti na kile kinachoonekana kwenye jamii, walisema wanajisikia furaha kuwasindikiza wake zao kliniki.

Walipohojiwa ni kitu gani kiliwasukuma kuwasindikiza wake zao kliniki, walisema walikuwa wanataka kufuatilia kwa ukaribu maendeleo ya afya ya mama na mtoto kwa ujumla.

Wanandoa #1

Richard Mwendilemo, 43, mkazi wa Mkuranga mkoani Pwani ni miongoni mwa wanaume wachache ambao siku hiyo aliongozana na mke wake kliniki.

Bwana Mwendilemo alikuwa amebeba mkoba wa mke wake kipindi chote cha mahojiano kuonyesha utayari alionao katika kumsaidia mkewe hospitalini hapo.

Alisisitiza kwamba mara nyingi amekuwa akimsindikiza kuhudhuria kliniki hospitalini hapo.

“Baada ya kugundua mke wangu kapata ujauzito, mwanzoni nilikuwa nashindwa kumuelewa tabia zake, ilikuwa ni changamoto kwakweli, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda nikaanza kuzoea ile hali yake. Kwasababu muda mwingine alikuwa ananigombeza bila sababu lakini sikuwahi kuchukulia tofauti zaidi ya utani tu,” alisema.

“Muda mwingine namtania ili kumfanya awe na furaha. Lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha mabadiliko ya tabia zake hazihathiri ukuaji wa mtoto tumboni,” alisema.

Akizungumzia kuhusu majukumu ya mwanaume kipindi cha ujauzito, Mwendilemo anasema majukumu yanayotekelezwa na mwanaume ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto.

“Binafsi naelewa kwamba ujauzito sio mzigo wa mwanamke peke yake, bali ni jukumu la wote wawili, mwanaume na mwanamke. Ni jukumu letu sote kuhakikisha maendeleo ya mtoto ambaye hajazaliwa na mama yake yanakuwa mazuri wakati wote wa kipindi cha ujauzito,” anasema.

Akiunga mkono maneno ya mume wake, Modesta Machengo (38), aanasema mumewe ni ‘mshauri mzuri’ japokuwa amekuwa akimuudhi mara kwa mara kutokana na ujauzito wake, hakuwahi kupunguza mapenzi na msaada kwake.

“Namshukuru Mungu kwa kunipa mwanaume huyu. Achilia mbali majukumu yake ya kila siku kama baba mwenye nyumba, amekuwa ni msaada mkubwa sana kwangu katika kipindi hiki cha ujauzito wangu, katika kipindi kama hiki wanawake wengi tunapenda kuona waume zetu wanatujali na kutusaidia, hakika mwanaume wangu ni mfano mzuri wa kuigwa,” alisema.

Wanandoa #2

Calvin Chezi (36), mkazi wa Chang’ombe jijini Dar es Salaam anasema, “Niliamua kumsindikiza mke wangu hapa hospitalini kuhudhuria kliniki ili niweze kufahamu maendeleo yake na mtoto kwa ukaribu zaidi.”

Alizungumza haya baada ya kufanya mahojiano na gazeti la Mwananchi akiwa eneo la wodi hiyo ya wazazi katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

Alipoulizwa kama ujauzito wa mke wake ulisababisha mabadiliko yoyote ya tabia, Chezi alisema, “Kusema ukweli, hajabadilika kitabia kipindi chote cha ujauzito wake, hali yake inaendelea vizuri tu.”

“Siku zote huwa najisikia faraja ninapomuona mume wangu amekaa karibu na mimi ninapokuja hapa hospitali kuhudhuria kliniki. Hii inanifanya niamini kwamba yuko tayari kunisaidia mimi na mtoto kama jambo lolote baya litajitokeza,” anasema Hasia Bitigo, mkewe Chazi baada ya kuhojiwa.

Wanandoa #3

Wakiwa wameshikana mikono wakati wa kuingia katika lango kuu la jengo la wazazi katika Hospitali ya Muhimbili, Vincent Balenge (28) na mke wake Sarah Atanas (27), wote wakazi wa Kimara Jijini Dar es Salaam, walipokelewa na muuguzi aliyekuwapo sehemu ya mapokezi.

Baadaye walielekezwa kuketi kwenye kiti wakati wanasubiri zamu yao ya kuingia chumba cha matibabu kwa ajili ya kuonana na daktari.

Gazeti la Mwananchi likatumia nafasi hiyo kufanya nao mahojiano kuhusu ushiriki wa wanaume katika kipindi cha ujauzito, na Balenge alisema; “Nikiwa baba mtarajiwa, nimekuja hapa kumsindikiza mke wangu kuhudhuria kliniki. Japokuwa ukweli ni kwamba nimebanwa na mambo mengi ya msingi, lakini nimeona kuna umuhimu mkubwa wa mimi kuwapo hapa na mke wangu.”

Alipoulizwa kama mke wake alibadilika tabia kipindi cha ujauzito, Balenge alisema; “Ni kweli tangu amepata ujauzito, nimekuwa nakumbana na mambo tofauti tofauti, lakini ninayamudu.”

“Muda mwingine anataka nimpeleke sehemu ambayo hatujawahi kwenda, nami nimekuwa nikifanya hivyo ili kumfurahisha. Mwanzoni kabla ya ujauzito hakuwa na hizo tabia.”

Kwa upande wake, Atanas alisema siku zote anafurahia msaada kutoka kwa mumewe hususani inapofikia suala la kuongozana naye kuhudhuria kliniki.

“Hali hii inanipa furaha kumuona mume wangu akiwa amekaa karibu na mimi nikija kuhudhuria kliniki na zaidi ni pale anaposikiliza kwa makini maelezo ya daktari tunapokuwa tunazungumza naye kuhusu matumizi ya dawa na aina ya vyakula inavyotakiwa kula. Hata tunapokuwa nyumbani, hunikumbusha kunywa dawa kulingana na maelezo aliyoyatoa daktari. Nawaomba wanaume wengine kuiga mfano wa mume wangu, tukumbuke ujauzito unakuja na matatizo mbalimbali ya kiafya, hivyo basi ni muhimu kwa akina baba kuwasaidia wenza wao wawapo katika kipindi hicho,” alisema.

Ushauri kwa akina baba watarajiwa

Meneja wa wodi ya wazazi Hospitali ya Muhimbili, Stella Medadi anasema ni vema kwa wanaume kufika kliniki na wake zao ili kuja kufahamu maendeleo ya afya ya mama nay a mtoto aliyeko tumboni.

Kwa kufanya hivyo, itawasaidia hata wao kujua nini kinachoendelea na inakuwa rahisi kuweza kumsaidia mjamzito awapo katika hali yoyote ile.

Anasema kwa sasa ni wanaume wachache sana hujitokeza hospitalini hapo kwa lengo la kuwasindikiza wake zao kipindi cha ujauzito.

“Kusema ukweli, idadi kubwa ya wanawake wanafika hapa peke yao. Wengi wao wanasindikizwa na ndugu zao. Kwetu sisi hii inatuathiri kwa namna moja au nyingine, kwasababu muda mwingine tunatakiwa kutoa baadhi ya maelekezo kwa baba wa mtoto, lakini tunashindwa kufanya hivyo kwa sababu wengi wao hawaongozani na wake zao wakati wa kliniki,” alisema.