(VIDEO) Sugu: Wanaodhani Mbeya Mjini ni fursa ya ajira wanajidanganya

Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (kushoto) akizungumza na waandishi wa gazeti hili katika studio za MCL Digital alipotembelea ofisi za Kampuni ya Mwananchi Communications (MCL), Tabata Relini jijini Dar es Salaam, jana. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Sugu alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi alipotembelea ofisi za gazeti hilo, Tabata Relini jijini Dar es Salaam jana.

Dar es Salaam. Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ amesema wanasiasa wanaodhani kuwa Jimbo la Mbeya Mjini ni fursa ya ajira wanajidanganwa na wanapoteza fedha zao.

Sugu alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi alipotembelea ofisi za gazeti hilo, Tabata Relini jijini Dar es Salaam juzi.

Pamoja na mambo mengine, aliulizwa kuhusu minong’ono ya watu wanaojipanga kuvaana naye katika ubunge wa Mbeya Mjini, akiwamo Naibu Spika, Dk Tulia Ackson.

Huku akiangua kicheko, Sugu alisema: “Mbeya Mjini ni sehemu tofauti sana. Napenda kuwashauri watu wengi ambao wanadhani kwamba Mbeya Mjini ni fursa ya ajira, haiko hivyo. Pale tuna majukumu ya kufanya, majukumu ambayo hayakufanywa toka uhuru mpaka tulipoingia kama Chadema kama Sugu mwaka 2010, mpaka sasa watu wanaona tofauti kilichofanyika tangu 2010 mpaka sasa,” alisema.

Mbunge huyo ambaye pia ni waziri Kivuli wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, alisema suala la Mbeya Mjini ni gumu na hivyo watu wanaokwenda kuwania jimbo hilo watakuwa wanadanganywa.

“Labda ni kwa sababu hawaijui Mbeya au kwa sababu hawakai Mbeya. Mtu anakwambia njoo hivi, njoo hivi, njoo ufutulishe, njoo ufanye hivi, njoo ufanye kile na kwa kuwa wewe unakuwa desperate (kufanya lolote) unataka kitu, unafanya kile unachoambiwa na wapambe, lakini ni uhakika watu wanapoteza fedha pale,” alisema.

Alipoulizwa ni mambo gani makubwa ambayo yanawafanya wananchi waone uongozi wake ni tofauti na miaka ya nyuma, Sugu alijibu kwa kuuliza swali: “Wewe jiulize kwa nini mimi naitwa rais. Ahaaa, aaa, yaani kabla mimi hujaniuliza hilo swali, ulitakiwa wewe ujiulize mwenyewe, kwa nini Mbeya wanasema Sugu ni rais. Najua wapo wengi hawapendi, lakini ndio iko hivyo. Kwa hiyo hawaniiti rais for nothing (bila sababu), kuna sababu, na ni zaidi ya mbili, kuna mambo mengi tu,” alisema.

Alisema kimsingi chini ya uongozi wake wameweza kuwafanya wananchi waone kwamba uongozi uko mikononi mwao, wanaweza kumfanya wanavyotaka, wanamwona kiongozi, wanakula naye raha na wanapata naye shida.

“Ni hicho tu, mengine yote ni majukumu. Siwezi hapa kusema tumejenga madaraja, tumejenga barabara, hayo ni majukumu. Huwezi kumsifikia kiongozi kwa kutekeleza majukumu yake,” alisema Sugu ambaye pia ni msanii wa muziki.

Alisema vitu vya ziada walivyovifanya ambavyo si vya kawaida kwa siasa za Tanzania wala za Afrika, ni kwamba wamepeleka uongozi mikononi mwa wananchi na hicho ndicho wananchi wanajivunia.

Mbunge huyo ambaye hivi karibuni alitoka jela alikokuwa anatumikia kifungo cha miezi mitano kwa kosa ya kutoa maneno ya kebehi kwa Rais, alizungumzia rufaa aliyokuwa amekata, ambayo haijasikilizwa akisema bado anaisubiri kwa hamu.

Alisema rufaa hiyo iko palepale kwa maana yeye na mwenzake walifanya utaratibu wote chini ya hati ya dharura, lakini mpaka leo (jana)hawajapata wito mahakamani.

“Na hii ndiyo inatia mashaka sana na uhuru wa mahakama zetu. Unajiuliza hiki kitu kiko hivi au kuna mtu anaingilia shughuli za mahakama,” alihoji. Alifafanua kuwa yeye na katibu wa Chadema Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga waliomba rufaa kwa hati ya dharura na kuambiwa wangeitwa ndani ya wiki mbili, lakini bado hawajaitwa.

“Wiki mbili zikaisha, tukakaa ndani zaidi ya siku 100, tumetoka na hadi leo ni zaidi ya mwezi bado hatujaitwa. Tunasubiri huu mkwamo unaosababisha tusiitwe ukiisha labda tutaitwa tusikilize rufaa yetu,” alisema.

Uchaguzi mdogo

Kuhusu uchaguzi ndogo unaoendelea katika Jimbo la Buyungu na kata 77, na kwa upande wa Mbeya ambako kuna kata moja wilayani Kyela, Sugu alisema “kwa kukomaa” watakwenda kusimama kama walivyofanya katika Kata ya Ibigi, Novemba mwaka jana.

Katika uchaguzi huo, Chadema ilishinda kata moja kati ya 43 zilizokwenda CCM huku ukizingirwa na malalamiko mengi ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu.

“Mambo si rahisi, tumekomaa kwa hatua ya sasa kwa maana ya kukwepa ‘figisu’ ambazo zinaendelea, mara pingamizi, mara andika ‘zinjanthropus’. Mimi hata nikipewa hilo neno siwezi kupatia zile herufi. Hata ukiambiwa niandike neno George, zile herufi za Kiingereza si watu wote wanaweza kupatia, na hii haina maana kwamba hujui kuandika,” alisema.

Kuhusu kwamba baadhi ya wagombea wameshindwa kujaza fomu, mbunge huyo alisema hilo haliwezekani na kwamba katika miaka 26 ya mfumo wa vyama vingi hata wao hawawezi kupeleka mgombea ambaye hajui kusoma na kuandika wala asiyeweza kujaza fomu.

Nini kilitokea hadi wagombea wao wakaenguliwa? “Nd’o hivyo, ni ‘figisu’. Kama alivyosema (Barack) Obama, uchaguzi sio tu kupiga kura na watu kutangazwa. Kuna mambo mengine. Uhuru wa habari, uhuru wa kukampeni, kushiriki hatua mbalimbali...Sasa kama unakwenda kurudisha fomu ukakutana na Green Guard wakakunyang’anya fomu, unataka mimi nifanye nini, nitupe mishale?” anahoji na kuongeza:

“Nafikiri hili suala la kusimamia amani pia wakati linapokuja suala la uchaguzi sisi ndilo linatuponza”.

Kwanini wasisue?

Alipoulizwa kama mambo ni magumu kwa nini wasisue uchaguzi, Sugu alisema: “Uchaguzi si mali ya Chadema ni mali ya wananchi. Sisi tunafanya eneo letu na kama tusingeshiriki haya yanayotokea tusingeyajua. Wangesema wamegombea peke yao na kupita bila kupingwa, tungejua mapungufu haya?”

Hata hivyo, alisema mtazamo wake na Chadema kwa ujumla kuhusu kushiriki uchaguzi unaangaza zaidi uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu mwaka 2020.

“Pale ndio tunapanga mipango ambayo siwezi kuisema hapa, ya kukabiliana na mwenendo wa demokrasia na kuvuruga uchaguzi, lakini kinachotupa matumaini ni kwamba nguvu wanayokuwa nayo kwenye uchaguzi mdogo hawatakuwa nayo kwenye uchaguzi mkuu,” alisema.

Alisema kwa mfano, wakati huo wa uchaguzi, Mbeya wakiwa matahalan na polisi 200 hawawezi kupambana na wapiga kura 200,000 au 150,000 watakaokuwa wameamua nani awe mbunge wao.

Mbunge huyo alitoa wito kwa kila mtu ambaye hafurahii mambo yanavyokwenda achukue nafasi yake kupambana na hali hiyo.

“Tusiseme tu Chadema hivi, Chadema vile. Leo hii anakamatwa Lema, anakamatwa Sugu anawekwa ndani, anapotea Saanane, leo hii amepotea pia Azory ambaye sio Chadema,” alisema.

Alipoulizwa walipanga mikakati gani ya kupambana na hali iliyopo, Sugu alisema hawawezi kupanga mikakati kwa kuwa matatizo hayo yanayojitokeza katika chaguzi ndogo yamekuwa yanaibuka kila mara lakini kwa sura tofauti. “Huwezi kupanga mikakati hasi, unapanga mikakati chanya ukiamini kwamba hii ni nchi ya kidemokrasia.

“Kwa hiyo wewe unakuwa na positive attitude, kwamba tuweke mgombea mzuri, tuendeshe kampeni nzuri, tuseme sera zetu vizuri wananchi watuelewe, lakini wenzako wanapanga mikakati hasi. Sasa wote tukipanga mikakati hasi tutazidi kuitumbukiza hii nchi katika lindi la matatizo. Ndio maana sisi tunajitahidi kuwa positive mpaka pale ambapo kiwango cha ubinadamu kitakaposhindwa,” alisema.

Sugu ambaye ni mwanamuziki mbali na kusema hataacha muziki, alisema shughuli za Mbeya na Taifa zinamchukulia muda mwingi zaidi na hivyo kushindwa kutoa nyimbo nyingi zaidi.