Sehemu ya barabara ya Nelson Mandela kufungwa kwa siku tatu

Muktasari:

Kufuatia matengenezo hayo, kuanzia  eneo la mataa ya Ubungo hadi Riverside (kama unatokea Mwenge kuelekea Buguruni), itafungwa kwa siku hizo, badala yake magari yatalazimika kupita upande wa pili wa barabara hiyo hiyo (inayotoka Buguruni kuelekea Ubungo)

Dar es Salaam. Kuanzia leo Ijumaa Julai 20, 2018 hadi Jumatatu Julai 23, 2018 watumiaji wa barabara ya Nelson Mandela jijini Dar es Salaam watakumbana na usumbufu kutokana na matengenezo yatakayoanza kufanyika katika barabara hiyo eneo la Ubungo.

 

Kufuatia matengenezo hayo, kuanzia  eneo la mataa ya Ubungo hadi Riverside (kama unatokea Mwenge kuelekea Buguruni), itafungwa kwa siku hizo, badala yake magari yatalazimika kupita upande wa pili wa barabara hiyo hiyo (inayotoka Buguruni kuelekea Ubungo).

 

Hayo yameelezwa katika taarifa iliyotolewa leo Julai 20, 2018 na kampuni ya CCECC inayojenga barabara za juu katika makutano ya Ubungo.

 

“CCECC inapenda kuwajulisha watumiaji wa barabara katika makutano ya Ubungo kuelekea Nelson Mandela (Riverside) kuwa siku ya Ijumaa Julai 20 kuanzia saa tano usiku hadi Jumatatu (Julai 23) ujenzi utakuwa unaendelea na watumiaji wa barabara hii watakuwa wanapita kama inavyoonekana kwenye mchoro huu,” imesema taarifa hiyo.