VIDEO: WHO yatoa Sh5.3 kusaidia magonjwa ya mlipuko

Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dk Odiele Onyeze (Kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu wa Afya Dk Mpoki Ulisubisya dawa na vifaa tiba vya utambuzi wa magonjwa ya mlipuko. Picha na Herieth Makwetta

Muktasari:

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, leo Julai 20,  Mwakilishi Mkaazi wa WHO Dk Adiele Onyeze amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya kugundua magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa msaada wa dawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Dola za Marekani 2.5 milioni sawa na Sh5.3 bilioni.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, leo Julai 20,  Mwakilishi Mkaazi wa WHO Dk Adiele Onyeze amesema vifaa hivyo ni kwa ajili ya kugundua magonjwa mbalimbali ya mlipuko.

 

Dk Onyeze amesema vitu hivyo vitaiongezea uwezo serikali katika kupambana na magonjwa hayo na kuiweka nchi katika usalama zaidi na hivyo kufikia malengo iliyojiwekea.

 

"Dawa na vifaa hivi ninkwa ajili ya kutambua kuchunguza na kudhibiti matatizo yanayojitokeza katika nchi yetu kwa kuhakikisha tunachukua hatua na tunasonga mbele," amesema.

 

Mara baada ya kupokea msaada huo Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubisya amesema msaada huo ni kwa ajili ya kupambana na magonjwa kama kipindupindu, Ebola, sumukuvu, kimeta, homa ya manjano, dengue na chikungunya.

 

"WHO wameweza kutusaidia kudhibiti kwa kutuletea vifaa vya ongezeko na jotomwili mwilini kabla ya hizi tulikuwa nazo 23 katika hizo tano zilikuwepo za watu kupita na zingine za kupima kawaida."amesema.

 

Amesema pia wamewaongezea vifaa kwa ajili ya kupimia Malaria na wataangalia yale magonjwa ambayo hayapewi kipaumbele, vilevile kutakuwa na mchango katika magonjwa ya trakoma.

 

"Baada ya kupata msaada huu sisi pamoja na  WHO tutakuwa na nafasi nzuri ya kupambana na magonjwa haya, kwani katika nchi  yetu tuna timu ambazo zipo tayari na kupitia msaada huu timu zetu zitakuwa tayari kupambana na magonjwa haya," amesema Dk Ulisubisya.