Kilio cha saruji Dar chatikisa kila kona, waziri atoa matumaini

Muktasari:

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kutokuwepo kwa saruji ya kutosha katika maduka ya vifaa vya ujenzi kwenye maeneo ya Mwenge, Tegeta na Buguruni.

Dar es Saalam. Wakazi wa Dar es Salaam wameanza kukumbana na uhaba wa saruji ambayo imepanda bei kutoka Sh13,500 hadi Sh18,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 50.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kutokuwepo kwa saruji ya kutosha katika maduka ya vifaa vya ujenzi kwenye maeneo ya Mwenge, Tegeta na Buguruni.

Mmiliki wa duka la Edward Chifu Hardware, anayefanya biashara hiyo Tegeta, Edward Chifu alisema kwa zaidi ya wiki mbili sasa hawajapata saruji kutoka kwa wazalishaji, licha ya kuagiza mara kadhaa.

“Jambo hilo limesababisha kupanda kwa bei ya saruji, hata hivyo hakuna sababu zilizowekwa wazi kwa nini usambazaji huo haufanyiki,” alisema Chifu na kuongeza kuwa, hata anakonunua kwa wauzaji wa jumla bidhaa hiyo imepanda bei kufikia Sh15,000 kwa mfuko. Mussa Idd anayeuza saruji eneo la Mwenge alisema hivi sasa imeadimika kutokana na Dangote kupunguza usambazaji. “Sasa Dangote anauza zaidi mikoani, hivyo hapa Dar es Salaam tunategemea simenti ya Nyati na Twiga, sasa Twiga naye ni kama amepunguza uzalishaji, Nyati anashindwa kukidhi mahitaji ya hapa ndiyo maana simenti inaadimika,” alisema Idd.

Mfayakazi wa kiwanda cha Wazo Hill ambacho huzalisha saruji ya Twiga aliyeomba jina lake lihifadhiwe, alisema wamepunguza uzalishaji kutokana na upungufu wa malighafi. “Kuna malighafi kutoka nje ya nchi inayoitwa clinker tunatumia katika uzalishaji, hivi sasa hazipatikani kwa wingi lakini bei ya saruji haijaongezeka, hivyo kuna uwezekano hata wa kusitisha uzalishaji,” alisema.

Baadhi ya wateja wanalalamikia uhaba huo kwa madai kuwa sasa wanalazimika kununua saruji kwa bei ghali. “Nanunua saruji kwa Sh20,000 ilimradi tu nimalizie ujenzi wangu. Hata hiyo ninaipata kutoka kwa watu ambao wametunza akiba, sio wauzaji,” alisema John Masawe anayeendelea na ujenzi wa nyumba eneo la Goba.

Wazungumzaji wa kampuni ya Lake Cement wanaozalisha saruji ya Nyati na Dangote wanaozalisha ile ya Dangote walipotafutwa ili kuzungumzia uhaba uliopo sokoni walikataa kuzungumza chochote.

Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage alisema tatizo lilikuwa ni matengenezo ya mitambo ya kuzalishia malighafi za simenti katika viwanda kadhaa, lakini sasa yamekamilika hivyo upatikanaji utarudia katika hali ya kawaida. “Twiga kesho au kesho kutwa wataanza uzalishaji, Dangote naye ameanza kuzalisha tani 4,100 hadi 4,500; Tembo tani 1,100 na Nyati tani 2,000. Hivyo tutakuwa na simenti ya kutosha,” alisema Mwijage.