Dunia yamlilia Koffi Annan, mchango wake duniani wakumbukwa

Geneva, Uswisi. Viongozi wa kitaifa na kimataifa wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Gutteress wameungana na wananchi wa mataifa yao kuomboleza kifo cha Katibu Mkuu mstaafu wa umoja huo, Kofi Annan.

Annan aliyekuwa kiongozi wa UN kuanzia 1997 hadi 2006, alifariki dunia jana mjini Geneva, Uswisi baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kiongozi huyo amefariki akiwa na umri wa miaka 80, huku akiacha alama ya utetezi wa amani duniani iliyomfanya kushinda tuzo ya amani ya Nobel (Nobel Peace prize)mwaka 2001.

Jana asubuhi, familia ya Annan iliandika kwenye ukurasa rasmi wa Twitter wa mwanadiplomasia huyo ikitoa taarifa za kifo chake.

“Mke wake, Nane na watoto wao Ama, Kojo na Nina walikuwa naye pamoja katika siku zake mwisho...familia inaomba faragha katika kipindi hiki cha msiba, utaratibu wa kuomboleza maisha yake utatangazwa hapo baadaye,” ilisomeka taarifa hiyo.

Saa chache baada ya kifo chake, Gutteress alitoa taarifa kwa vyombo vya habari akiomboleza kifo cha Annan akimtaja kuwa msimamizi elekezi wa mema.

“Nimezipokea kwa huzuni taarifa za kifo cha Koffi Annan. Kwa namna nyingi, Koffi Annan alikuwa sehemu ya UN. Aliipandisha UN katika viwango vya juu na kuiongoza taasisi hii katika nyakati mpya na heshima isiyoweza kufananishwa,” ilisema taarifa ya Guterres.

“Kama ilivyokuwa kwa wengi, nilijisikia fahari kumuita Kofi Annan rafiki mzuri na mwalimu. Niliguswa sana na imani yake kwangu kwa kunichagua mimi kuwa kamishna wa UN anayesimamia masuala ya wakimbizi chini ya uongozi wake.”

Guterres alisema Annan aliendelea kuwa mtu anayetegemewa kwa ushauri na hekima ndani na nje ya umoja huo.

“Ninajua sikuwa peke yangu, aliwasaidia wengi, kila mahali aliwapa watu nafasi kuzungumza naye, alipewa nafasi ya kuwatatulia matatizo wengine.”

Amesema kuwa Annan hakuacha kuienzi thamani ya UN na hivyo amewaachia urithi ambao utaendeleza uongozi wake wa kweli watu kwa wote.

“Nawapa pole mke wa Annan, Nane Annan na familia nzima na wote wanaoomboleza kifo cha kiongozi huyu wa Afrika ambaye amekuwa shujaa wa amani duniani.”

Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter akisema amesikitishwa na kifo kiongozi huyo. “Ni kiongozi shupavu aliyeibadili UN. Ana mchango mkubwa katika kuhakikisha aliuacha ulimwengu sehemu nzuri kuliko ile ya wakati aliozaliwa,” aliandika May.

Wengine waliomlilia Annan ni Mratibu Mkazi wa Shirika la Maendeleo la UN nchini Tanzania, Alvaro Rodrigues aliyeandika kwenye ukurasa wa Twitter akisema, “Tunaomboleza kifo cha Annan.”

Mwanasiasa wa upinzaji nchini Afrika Kusini, Julius Malema aaliandika: “Tunakuheshimu mheshimiwa.”

Raia huyo wa Ghana anakumbukwa zaidi kwa juhudi zake za kutafuta amani nchini Syria, Iraq na mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi duniani kote.