Diwani wa Chadema Hai, ajiuzulu

Muktasari:

Ataja sababu ni Chadema kutoridhishwa na demokrasia ndani ya Chadema.

Dar es Salaam. Diwani wa Chadema kata ya Masama Rundugai, Elibariki Mbise, amejiuzulu uanachama na udiwani wake leo Agosti 21 na kutangaza kujiunga na CCM.

Katika barua yake aliyoiandika kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Mbise amesema sababu za kujiuzulu wadhifa huo ni kutoridhishwa na  demokrasia ya chama hicho.

 “Nimejiuzulu nafasi zangu zote nilizokuwa natumikia ndani ya chama hiki kwa sababu hakina demokrasia pana ambayo inaweza ikaisaidia jamii katika kutatua matatizo na kuleta maendeleo ya kweli,” amesema.

Amesema sababu nyingine ni Chadema kupinga na kutokukubali juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali ya awamu ya tano na Rais John Magufuli.

Mbise ameandika barua hiyo na kupeleka nakala kwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya. Nakala nyingine zimepelekwa  kwa Katibu wa Chadema, Hai, Katibu wa CCM,  Hai  na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.