Mbunge wa nane upinzani ajiunga CCM

Muktasari:

Chadema kimesema kinafuatiria taarifa za mbunge wake wa Babati Mjini, Pauline Gekul za kujizulu na kujiunga na CCM leo Oktoba 13,2018.

Dar es Salaam. Habari ambazo si rasmi ni kwamba Mbunge wa Babati Mjini (Chadema), Pauline Gekul ametangaza kujiuzulu wadhifa huo na kujiunga na CCM.

Barua inayosambaa kwa kasi  mitandaoni kuanzia saa 4.20 usiku ikionyesha kwenda kwa Spika wa Bunge Job Ndugai ikiwa imesainiwa na Gekul anasema amejiuzulu uanachama na ubunge wake.

Jitihada za kumpata Gekul kuzungumzia undani wa barua hiyo zimegonga mwamba kwani simu zake za kiganjani hazipatikani huku viongozi wa chama chake cha Chadema wakishindwa kuthibitisha kama ni kweli au la.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa akizungumza na Mwananchi amesema na yeye anaiona barua hiyo inasambaa mitandaoni.

"Mimi mwenyewe naiona barua mtandaoni na ninamtafuta katika simu zake hapatikani lakini katika baadhi ya makundi yetu kajitoa mwenyewe na mengine alijitoa kitambo kidogo na inaweza kuwa  ishara ni kweli," amesema Golugwa

Naye Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema,"Mimi mwenyewe namtafuta lakini simpati. Lakini ukiangalia hii barua inafanana naya (James) Millya hadi nukta."

Mrema anasema wanafuatilia kujua ukweli wa taarifa hizo kwa kina.

Ikiwa ni kweli Gekul kajiuzulu, atakuwa mbunge wa nane wa upinzani na tisa wa Bunge la 11 chini ya Spika Ndugai kujiuzulu.

Lazaro Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kupitia CCM alijiuzulu na kujiunga na Chadema.

Waliojiuzulu na kutimukia CCM walikopitishwa na kugombea na sasa ni wabunge ni; Maulid Mtulia (Kinondoni-CUF) na Dk Godwin Mollel (Siha-Chadema).

Wanaosubiri kuapishwa ni; Mwita Waitara (Ukonga-Chadema) na Julius Kalanga (Monduli-Chadema) huku Zuberi Kuchauka (Liwale-CUF) huenda akaibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika leo Jumamosi Oktoba 13,2018.

Wengine waliojizuli hivi karibuni ni; Mwarya Chacha (Serengeti-Chadema) na James Milly wa Simanjiro naye Chadema.