Wakili Takukuru akwamisha kesi ya Tido Mhando

Muktasari:

Leo ni mara ya pili kesi hiyo inaahirishwa ikiwa katika hatua za mshtakiwa kuulizwa maswali.


Dar es Salaam. Kesi ya aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando imekwama kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumanne Oktoba 16, 2018.

Leo,  Tido alipaswa kuulizwa maswali na upande wa mashtaka dhidi ya utetezi alioutoa katika mahakama hiyo lakini imeshindikana baada ya wakili  wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai kutokuwapo mahakamani, ikielezwa kuwa yupo nje ya Dar es Salaam.

Leo ni mara ya pili kesi hiyo inaahirishwa ikiwa katika hatua za mshtakiwa kuulizwa maswali.

Oktoba 9, 2018 kesi hiyo iliahirishwa baada ya Swai kuwa na udhuru.

Tido ambaye anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1milioni  alitoa utetezi wake dhidi mashtaka hayo, Septemba 20, 2018.

Katika utetezi wake huo  aliongozwa na mawakili wake, Dk Ramadhani Maleta na Martin Matunda.

Wakili wa Takukuru, Dismas Mganyizi amedai mahakamani hapo mbele Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma  Shaidi kuwa Swai  amesafiri kwenda Musoma na kuomba kesi hiyo kuahirishwa.

Hakimu Shaidi ameridhia na kuahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 30, 2018 na kwamba siku hiyo Tido ataanza kuulizwa maswali na upande huo wa mashtaka dhidi ya utetezi wake alioutoa.

Miongoni mwa mashahidi  wa upande wa mashtaka ambao wametoa ushahidi katika kesi hiyo ni ofisa uchunguzi wa Takukuru, Victor Lesuya, mwanasheria wa TBC, Gwakisa Mlawa, mkurugenzi mkuu mstaafu wa TBC, Clement Mshana na Dominic Maundi.

Katika kesi hiyo inadaiwa Juni 16, 2008, akiwa  Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),  Tido kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha na utangazaji wa vipindi vya televisheni kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila ya kupitisha zabuni, kitu ambacho ni kinyume na Sheria ya Manunuzi na kuinufaisha BVl.

Katika shtaka la pili, Tido anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake Juni 20, 2008 aliposaini makubaliano kwa utangazaji wa digitali duniani kati ya TBC na BVl.

Katika shtaka la tatu, anadaiwa Agosti 11, 2008 na Septemba 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa ununuzi, usambazaji kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.

Katika shtaka la nne, anadaiwa kuwa  Novemba 16, 2008 akiwa Dubai, Tido alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano kwa kuendesha miundombinu ya utangazaji (DTT Broadcast  Infrastructure) kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.

Katika shtaka la mwisho,  anadaiwa kuwa kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008 akiwa UAE, Tido aliisababishia TBC  hasara ya Sh887,122,219.19. Tido yupo nje kwa dhamana.