Majina ya watumishi waliogoma kuhamia kituo cha kazi yatua kwa Jafo

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo amemkabidhi Waziri wa Tamisemi majina ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ili wachukuliwe hatua baada ya kugoma kwenda katika vituo vyao vya kazi na kuendelea kuishi mjini Dodoma

 


Dodoma. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemkabidhi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo orodha ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bahi ili awachukulie hatua baada ya kugoma kuhamia katika kituo chao cha kazi na kuendelea kuishi jijini Dodoma.

Amemkabidhi orodha hiyo leo baada ya mkuu wa wilaya hiyo, Mwanahamisi Mukunda kusoma taarifa ya wilaya.

Katika taarifa hiyo pamoja na mambo mengine, Mwanahamisi alieleza kuwa watumishi wote wameshahamia kwenye kituo chao cha kazi na wanaishi maeneo hayo. Waziri Mkuu alikuwa katika kikao na watumishi wa halmashuri hiyo.

“Mkuu wa wilaya umedanganywa watumishi bado wanaishi jijini Dodoma, walichokifanya baadhi wamejiunga watatu na wamekodi chumba kimoja. Namkabidhi Waziri wa Tamisemi orodha ya watumishi hawa ambao wamegoma kuishi kwenye kituo chao cha kazi ili uwashughulikie,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wamegoma kuhamia katika kituo chao cha kazi licha ya Serikali kuwataka kufanya hivyo.

”Maelekezo hatuyatoi kwa ajili ya kujifurahisha bali tunataka utekelezaji ufanyike ili wananchi waweze kuhudumiwa ipasavyo,” alisema.

Juni 27  Majaliwa wakati akizindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzi data ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, aliwaagiza watumishi wa halmashauri hiyo wanaoishi nje ya kituo chao cha kazi wahamie kituoni kwao.

Leo  Waziri Mkuu alikagua mradi wa ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari ya Mpalanga yenye uwezo wa kukaliwa na walimu sita, ambapo alisema ameridhishwa na ujenzi huo. Mradi huo unagharimu zaidi ya Sh.140 milioni.

Pia amezindua daraja la Chipanga ambalo ujenzi wake umegharimu Sh2.18 bilioni na kisha alitembelea kituo cha afya cha Bahi ambako alikagua wodi ya wazazi na kuzungumza na akinamama ambao waliishukuru Serikali kwa kuboresha huduma za afya.