Wapo wapi waliofanya uhalifu huu

Muktasari:

  • Jeshi la Polisi limekuwa likieleza jitihada zake za kuwasaka waliomteka na kisha kumuachia mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’,  lakini bado wana kazi nyingine ambayo haijakamilika ya kuwatia nguvuni watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali yakiwamo ya utekaji na kupotea kwa watu


Dar es Salaam. Wakati Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro akisema polisi watahakikisha wanawapata waliohusika kumteka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohammed Dewji ‘Mo’, bado wana kazi nyingine ambayo haijakamilika ya kuwatia nguvuni watuhumiwa wengine wanaodaiwa kuhusika katika matukio mbalimbali yakiwamo ya utekaji na kupotea kwa watu.

Pia, wapo watuhumiwa wengine waliohusika katika tukio la kumjeruhi kwa risasi mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu pamoja na mtu aliyehusika kumtishia kwa bastora aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye.

Dewji aliyetekwa Oktoba 11 katika Hoteli ya Colosseum, Oysterbay jijini Dar es Salaam, alipatikana siku ya Jumamosi saa 7:30 usiku baada ya kutelekezwa na watekaji maeneo ya viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam.

Oktoba 13, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam alisema watu 75 walitekwa katika miaka mitatu iliyopita, ingawa wengi wao walipatikana.

Kutokana na matukio hayo, Lugola alisema Serikali itahakikisha watu ambao hawajapatikana wanapatikana na waliohusika wanachukuliwa hatua kali.

Huku kupatikana kwa Mo Dewji ikiwa ni habari nzuri, Sirro alisema licha ya hatua hiyo, “mchezo ndiyo kwanza umeanza.”

Mkuu huyo wa polisi alinukuliwa akisema kazi iliyobaki ni kuwasaka wahusika ili kuwaonyesha kuwa Tanzania si mahali salama kwa wahalifu.

Alisema, “Unapoanza mbio lazima zifike mwisho, watakapokwenda na sisi tutakwenda, hatuwezi kuwaachia, tukiwaacha watajipanga upya.”

Jeshi hilo lililoweka nguvu kubwa ya kuhakikisha mfanyabiashara huyo tajiri Afrika kwa vijana anapatikana, limekuwa kimya kwa baadhi ya matukio na kushindwa kutoa ama taarifa za uchunguzi au hata watuhumiwa waliohusika.

Mwananchi linachambua matukio ambayo mpaka sasa ama watuhumiwa hawajapatikana au yamechukua muda mrefu katika uchunguzi mikononi mwa polisi.

Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na kutekwa kupotea kwa mwenyekiti wa Halmashauri ya Kibondo, Simon Kanguye; kada wa Chadema, Ben Saanane; mwandishi wa habari wa kujitegemea wa Mwananchi, Azory Gwanda na mtoto Idrissa Ally ambayo upelelezi wake haujakamilika na watuhumiwa kuwekwa hadharani.

Waliomteka Saanane

Ben Saanane aliyekuwa msaidizi wa mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipotea katika mazingira ya kutatanisha Novemba 18, 2016 na hadi jana ilikuwa haijafahamika kama alitekwa au kupotea.

Saanane ametimiza siku 705 sawa na mwaka mmoja na miezi 11 tangu alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha.

Novemba 14, 2016 ndiyo ilikuwa siku ya mwisho kwa Saanane kuonekana katika ofisi za makao makuu ya Chadema zilizopo mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam ambako alitumia muda wake mwingi. Siku hiyo alisaini kitabu cha mahudhurio ya wafanyakazi na kufanya shughuli zake za kichama.

Polisi wamsubiri Lissu arejee

Licha ya kutimiza mwaka mmoja tangu Lissu kushambuliwa kwa risasi, polisi wamenukuliwa wakisema wanamsubiri mbunge huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji kwa matibabu pamoja na dereva wake warejee nchini.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Boaz aliliambia Mwananchi kuwa mara tu watakapowasili nchini jeshi hilo litafanya nao mahojiano kwa sababu ni mashahidi muhimu.

Kufuatia hatua hiyo mpaka sasa waliohusika katika jaribio hilo la kutaka kumuua mbunge huyo hawajatiwa nguvuni. Mwingine ni Kanguye aliyetoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 20, 2017.

Jana, mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya Kibondo alitimiza siku 459 (sawa na mwaka mmoja na miezi miwili) tangu alipotoweka machoni mwa ndugu, jamaa na marafiki zake.

Kwa mujibu wa mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa mwaka 2018/2019 huku akizungumzia matukio ya utekaji na kupotea kwa watu, alisema Kanguye aliitwa katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Kibondo kukutana na DSO na tangu hapo hajaonekana.

Watumiwa wengine ambao hawajapatikana mpaka sasa ni wale waliohusika kumteka Azory aliyetekwa na watu wasiojulikana Novemba 21, 2017.

Hadi jana, Azory alikuwa ametimiza siku 335 (sawa na miezi 10 na siku 29) tangu alipochukuliwa.

Mpaka sasa si mwandishi huyo wala waliohusika kufanya utekaji huo waliotiwa nguvuni na polisi.

Mwingine ni mtuhumiwa aliyemteka mtoto Idrisa Ally (13), aliyechukuliwa ‘kimafia’ na mtu asiyejulikana akiwa anacheza nyumbani kwao eneo la Tegeta Masaiti jijini Dar es Salaam.

Idrissa, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Princes Gate, alichukuliwa saa 11 jioni akiwa anacheza na wenzake na hadi jana alikuwa ametimiza siku 24 hajaonekana.

Mtoto huyo alichukuliwa na dereva mwanamume aliyekuwa akiendesha gari aina ya Toyota IST, ambaye baada ya kuwafukuza marafiki wa Idrissa, alitoa kichupa kidogo kinachodhaniwa kuuwa ni ‘spray’ na kumpulizia mtoto huyo kisha akamuingiza mlango wa nyuma wa gari lake.

Lugola na takwimu

Akizungumza hivi karibuni, Waziri Lugola alisema kuanzia Januari hadi Oktoba 11, watu 21 walitekwa na kati yao 17 walipatikana wakiwa hai huku wanne hawakuwa wamepatikana hadi siku hiyo alipozungumza na waandishi wa habari Oktoba 14.

Alisema watuhumiwa 10 walikamatwa na kufikishwa mahakamani.

Polisi wasione aibu kusaidiwa

Akizungumzia kauli ya IGP Sirro, mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema chama chake kinaonyesha masikitiko makubwa kwa jeshi hilo kwa kushindwa kuwapata waliohusika katika matukio mbalimabili wakiwamo waliomjeruhi Lissu. “Polisi leo wanajigamba watahakikisha watuhimiwa waliomteka Mo wanapatikana, lakini mpaka sasa ni mwaka mmoja na zaidi hakuna aliyehojiwa au taarifa yoyote kuhusiana na waliomjeruhi Lissu,” alisema.

Mrema alisema si tukio hilo pekee, bali wapo pia waliohusika kumteka Azory na Saanane ambao hawajatiwa nguvuni mpaka sasa na kuhoji uwezo wa polisi kushughulikia watuhumiwa waliomteka Mo.

“Tulitamani Jeshi la Polisi wafanye jitihada sawa katika matukio yote na si kuchagua aina ya matukio na ku-deal nayo na matokeo yake taarifa za maofisa wake zinatofautiana.”

Aliongeza kuwa, “Siamini kama hilo jambo linaweza kufanikiwa, hivi kweli watu wanakuja kumteka Mo katikati ya ulinzi mkali kutokana na eneo lenyewe kuzungukwa na nyumba za wakubwa na wanamrejesha kisha kuondoka bila kuonekana, leo mtuambie kwamba mtawashika?”

Mrema alisema polisi haina budi kukubali kuomba msaada kutoka nje kama ilivyoamua kuushirikisha umoja wa majeshi ya polisi duniani (Interpol) katika suala la mfanyabiashara huyo.

Mkazi wa Ubungo jijini Dar es Salaam, Masoud Jineshi alisema polisi wanapaswa kufanya kazi usiku na mchana katika matukio ya aina hiyo ili kuongeza imani kubwa ya wananchi dhidi yao.

“Bado nawaamini polisi, na bado naamini wanafanya kazi kubwa, lakini ukimya katika matukio ya aina hii inaibua maswali,” alisema.

Marrystella Aloyce wa Kigamboni alimshauri IGP Sirro kuwabana zaidi wasaidizi wake ili waongeze juhudi za kuwasaka Watanzania waliopotea na kuwakamata.

“Akifanya hivyo, IGP atakuwa mtu wa watu kwelikweli. Bado nafasi anayo,” alisema Marrystella.