ATCL yaendelea kuzivutia kasi safari za Dreamliner kwenda India

Muktasari:

Ni katika mpango  wa kuendelea kuboresha mikakati yake ya kibiashara, kiutendaji na kiuendeshaji

Dar es Salaam. Licha ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), kurejeshwa katika Shirikisho la Mashirika ya Ndege Duniani (IATA), limeshindwa kuweka wazi tarehe ambayo litaanza safari zake za kwenda Mumbai, India.

ATCL iliondolewa katika shirikisho hilo mwaka 2009 baada ya kuelemewa na mzigo wa madeni, lakini tangu lilipofufuliwa upya 2016 limekuwa likipambana kurejea upya katika uanachama na hivi karibuni limefanikiwa, hivyo kupata fursa ya kuuza tiketi zake kimataifa.

Mkurugenzi mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alilieleza Mwananchi kuwa bado kuna mambo wanayashughulikia ili kuanza safari hizo na muda ukifika wataeleza ili abiria waanze kununua tiketi.

Julai mwaka huu, wakati ATCL ikipokea ndege aina ya Boeing 787-8 Dreamliner ilitangaza safari za kwenda Mumbai zingeanza Septemba, lakini haikuwa hivyo badala yake walieleza itakuwa siku yoyote mwezi Novemba.

Shauku ya kuanza kwa safari hizo ni kutokana na kutokuwepo kwa ndege za moja kwa moja kwenda katika eneo hilo.

Mara ya mwisho kufanyika kwa safari za Mumbai zilikuwa zikifanywa na Shirika la Ndege la India (Air India) ambalo sasa halifanyi.

Kwa mujibu wa matangazo mbalimbali ya ATCL katika vyombo vya habari litakuwa likifanya safari tatu kwa wiki-Jumatano, Ijumaa na Jumapili-ikitumia Boeing 787-8 Dreamliner.

Bei iliyotangazwa kwa safari za Mumbai ni Dola 286 za Marekani (zaidi ya Sh653,166) kwa safari ya ama kwenda au kurudi na Dola455 (zaidi ya Sh1 milioni) kwa safari ya kwenda na kurudi.

Hivi sasa ATCL ina ndege nne kati yake, tatu zikiwa ni aina ya Bomberdier Q400 na moja aina ya Boeing 787-8 Dreamliner.

Ndege mpya mbili aina ya Airbus A220-300 zinatarajiwa kuwasili nchini kabla ya mwisho wa mwaka huu na Dreamliner nyingine mwakani.

Hali ya biashara ya ATCL

Kwa sasa ATCL imetawala soko la ndani kwa zaidi ya asilimia 24 ikisafirisha abiria katika mikoa 12 na katika nchi za Comoro, Burundi na Uganda.

Vilevile shirika hilo limefanikiwa kupunguza kiwango cha hasara lilichokuwa linapata miaka ya nyuma kutoka Sh14.2 bilioni mwaka 2016 hadi Sh4.3 bilioni mwaka 2017, huku likiongeza mapato hadi Sh4.5 bilioni kwa mwezi katika kipindi hicho.