Wakili maarufu Matunda afariki dunia, azikwa Dar

Muktasari:

Wakili Matunda ambaye wakati wa uhai wake alishiriki kuendesha kesi mbalimbali zikiwemo za watu maarufu, alifariki Jumatatu katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo maeneo ya Mwenge jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wakili maarufu jijini Dar es Salaam, Martin Depores Matunda amefariki dunia jijini hapa, huku taarifa zikieleza kuwa aliaga dunia ghafla wakati akijiandaa kwenda kazini.

Wakili Matunda ambaye wakati wa uhai wake alishiriki kuendesha kesi mbalimbali zikiwemo za watu maarufu, alifariki Jumatatu katika Hospitali ya Mama Ngoma.

Taarifa za kifo cha wakili huyo ambaye alikuwa mwanachama wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), zimetangazwa pia kwenye tovuti ya TLS na kuthibitishwa na Ofisa Habari wa chama hicho, Salima Mseta.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mseta alisema Matunda alifariki ghafla siku hiyo nyumbani kwake Sinza E (Kwa Remmy), mtaa wa Muungano, baada ya kuanguka bafuni akiwa anaoga na alizikwa jana saa nne asubuhi.

“Alianguka tu ghafla bafuni akiwa anaoga ili ajiandae kwenda kazini,” alisema Mseta.

“Ghafla alianguka chini mara akaanza kutokwa damu na walipompeleka hospitalini akawa amefariki dunia.”

Matunda alisajiliwa kuwa wakili wa kujitegemea wa Mahakama Kuu na mahakama za chini (isipokuwa mahakama za mwanzo) Desemba 15, 2000 na kupewa namba ya usajili 852, ikimaanisha alikuwa wakili wa 852 katika orodha ya mawakili wote nchini.

Miongoni mwa kesi alizosimamia wakili huyo ni pamoja na ya aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando, ya matumizi mabaya ya madaraka inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo ambayo iko katika hatua za mwisho, Wakili Matunda alianza kumtetea Mhando akiungana na Wakili Ramadhani Maleta, wakati ikiwa katika hatua ya utetezi.

Ni yeye Matunda aliyemuongoza Mhando kutoa ushahidi wa utetezi.

Wakili huyo alikuwa akitarajiwa kushiriki katika hatua za mwisho kabisa za kesi hiyo ambazo ni kuwasilisha hoja za mwisho kuishawishi mahakama imuone Mhando kuwa hana hatia katika mashtaka yanayomkabili.

Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, anayesikiliza kesi hiyo amepanga mawakili wa pande zote katika kesi hiyo (upande wa mashtaka na ule wa utetezi) kuwasilisha hoja zao za mwisho, Novemba 15 kabla ya kupanga tarehe ya hukumu.