Upelelezi wa Sethi, Rugemalira bado, Takukuru yamhoji Sethi

Muktasari:

Upelelezi wa kesi inayomkabili Harbinder Sethi na James Rugemalira katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Novemba 22, 2018-11-08

Dar es Salaam. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru)  imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa jana Jumatano Novemba 7, 2018 walifanikiwa kuchukua maelezo ya mshtakiwa Harbinder Sethi.

Wakili wa Takukuru, Leonard Swai ameyaeleza hayo leo Alhamisi Novemba 8, 2018 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili Swai amesema mahakamani hapo kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado haujakamilika na kwamba jana walifanikiwa kuchukua maelezo ya Sethi na kwamba wanaendelea na hatua zinazofuata za upelelezi.

Kwa upande wa Wakili wa Sethi aliyekuwepo mahakamani hapo, David Chillo ameutaka upande wa mashtaka kuongeza spidi ya upelelezi.

Baada ya pande hizo mbili kueleza hayo, Hakimu Shaidi ameiahirisha kesi hiyo hadi Novemba 22, 2018 kwa ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika ama la.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi kwa kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu , kughushi,  kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kutakatisha fedha na kuisababishia Serikali hasara ya Dola za Marekani 22.1 milioni na Sh309.4 bilioni.

Washtakiwa hao wapo rumande kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana.