2017 ilivyorudisha siasa za 1992

Muktasari:

Wananchi walitangaziwa kundi kubwa la wanachama, lakini waliokuwa wanajitokeza jukwaani walikuwa wachache.

Dar es Salaam. Mwaka 2017 unamalizika kwa kurejesha kumbukumbu za mwanzoni mwa siasa za vyama vingi wakati nchi ilipokuwa ikiingia kwenye uchaguzi wa kwanza tangu siasa za ushindani ziliporejeshwa mwaka 1992.

Habari zilizotawala wakati huo zilikuwa ni taarifa zilizotolewa na viongozi wa vyama kuwa wamerejeshewa kadi za idadi kubwa ya wanachama waliokuwa wamejiunga ama na CCM, NCCR-Mageuzi CUF au Chadema.

Wananchi walitangaziwa kundi kubwa la wanachama, lakini waliokuwa wanajitokeza jukwaani walikuwa wachache.

Miaka 23 baadaye, hali hiyo inaonekana kujirudia, tena kwa nguvu kubwa.

Wakati ule ilikuwa ni wanachama wengi wasiofahamika na ambao waliwakilishwa na wachache kurudisha kadi za vyama walikotoka, lakini safari hii ni viongozi; tena walioshika nafasi kubwa kama za udiwani na ubunge ndio wanaotangaza kujivua nyadhifa zao na kuhamia chama ambacho wanaona kinawafaa. Ndivyo mwaka 2017 ulivyoisha kwa kishindo hicho.

Ni dhahiri ni dhahiri mazingira ya kufanyia siasa yamebadilika, lakini hakuna aliyeweza kueleza sababu za wimbi hilo kutokea wakati huu ambao siasa za ushindani zilitakiwa kuwa zimekomaa baada ya vyama kushiriki chaguzi tano tangu mwaka 1995 wakati ulipofanyika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Lazaro Nyalandu, aliyekuwa mgunge wa Singida Kaskazini na ambaye uamuzi wake wa kujivua ubunge ulitikisa, alisema ameamua kuhamia upinzani ili kuongeza nguvu ya kupigania demokrasia, kupambana na ukiukwaji wa haki za binadamu, dhuluma na kupigania Katiba Mpya.

Wale wanaohama upinzani kwenda CCM wanasema wanamuunga mkono Rais John Magufuli kwa kuwa anatekeleza yale waliyowaahidi wananchi, wengine wakisema ajenda ya ufisadi haina nguvu tena kwa kuwa Rais anaishughulikia.

“Nadhani ni watu kutojua misingi ya vyama,” alisema mbunge wa Temeke (CUF), Mohamed Mtolea katika mahojiano na kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Azam TV wiki iliyopita.

“Wengi hawaelewi kuwa itikadi ndio msingi wa chama chochote. Mtu unajiunga na chama kwa sababu unakubaliana na itikadi ya chama hicho, si ajenda.

“Ajenda huja na kupita kulingana na mazingira ya wakati huo. Pia ubinafsi unasababisha mtu kuwasahau waliokuchagua na kuweka masilahi yako binafsi mbele.

Safari hii siasa za hamahama zilianzia Arusha, mkoa ambao unaaminika kuwa ni ngome ya Chadema, baada ya baadhi ya madiwani wa chama hicho kujivua nyadhifa zao kwa sababu ile ya kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli.

Wakati madiwani hao wakijiengua, mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema walituhumu kuwa kuna rushwa inatumika na akawanyooshea kidole viongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.

Lakini hali ikaendelea hadi kufikia madiwani sita na baadaye wimbi hilo kuhamia mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Hai ambayo mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ndiye mbunge wa jimbo hilo.

Wakati hali ikionekana kutulia, Nasari na Lema walitangaza kuwa wana ushahidi wote wa jinsi rushwa ilivyotumika kuwarubuni madiwani hao, wakitamba kuwa hakuna kinachoweza kufanyika ofisi za halmashauri ambacho hawataweza kukijua.

Hawakuishia kutoa maneno matupu, bali walitoa ushahidi wa picha za video kwa waandishi wa habari zikimuonyesha aliyekuwa mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti na watendaji wengine wa halmashauri, wakifanya maongezi na madiwani hao.

Madiwani hao walipokewa na Rais John Magufuli wakati wa sherehe za kukamisheni maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Baadaye waliwasilisha video hizo Takukuru, lakini siku chache baadaye Mnyeti aliteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Manyara.

Madiwani waliojiengua ni Solomon Laizer (Ngabobo), Credo Kifukwe (Murieti), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (viti maalumu).

Mtikisiko wa madiwani hao, ulizimwa na uamuzi wa Nyalandu kujivua ubunge na uanachama wa CCM Oktoba 30 akiwa Arusha, akisema haridhishwi na mwenendo wa kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa haki za binadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya Watanzania.

Alitaja sababu nyingine kuwa ni kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya mihimili ya dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa kutunga sheria na kuisimamia Serikali kutofanyika kwa uhuru ulioainishwa na kuwekwa bayana Kikatiba.

Alitaja pia kutokuwapo kwa Katiba Mpya kuwa kunaifanya mihimili ya dola iingiliane na CCM kushindwa kuisimamia Serikali.

Alikuwa ni mbunge wa kwanza baada ya miaka kadhaa kuamua kujivua wadhifa wake kwa sababu ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama badala ya kulazimishwa na hali ya kutoelewana na viongozi kama ilivyotokea kwa wabunge wengine waliojivua uanachama.

Kuondoka kwa Nyalandu kulifuatiwa na ukimya ambao hata hivyo, ulitoweka baada ya kundi jingine la wanasiasa, kuamua kurejea CCM likiongozwa na waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ambaye alihamia CCM mwaka 2015 wakati wa wimbi lililomfuata aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Masha na wenzake walitambulishwa katika kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu. Wengine ni aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chadema (Bavicha), Petrobras Katambi na wanachama wa zamani wa ACT Wazalendo, Albert Msando, Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo. Wote walipata nafasi isiyo ya kawaida ya kuhutubia kikao hicho cha pili kwa ukubwa cha CCM.

Kama hiyo haitoshi, Novemba 22 aliyekuwa kada wa Chadema, David Kafulila alikihama chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM.

Siku mbili baadaye alikabidhiwa kadi ya CCM na Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mkutano wa kumnadi aliyekuwa mgombea wa udiwani wa chama hicho, Kata ya Mbweni, Dar es Salaam.

Kafulila aliwahi kuwa mwanachama wa Chadema kisha akufuzwa baadaye akajiunga na NCCR Mageuzi ambako alipata ubunge wa Kigoma Kusini (2010/15) na baada ya kupoteza jimbo hilo, alirejea Chadema 2016, akisema anaenda kuungana na watu ambao sauti zao zinafanana.

Baada ya Kafulila, aliyekuwa mbunge wa Kinondoni kwa tiketi ya CUF-Lipumba, Maulid Mtulia alijivua wadhifa huo na kujiunga CCM, akiwa na sababu ileile ya kuunga mkono juhudi za Rais.

Mtulia alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa mambo yote waliyoahidi tayari yanafanywa vizuri zaidi na CCM hivyo ni vigumu kuwa mpinzani.

Wiki iliyopita, aliyekuwa mwenyekiti wa ACT-Wazalendo ambaye sasa ni mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alitangaza kujiunga na CCM katika mkutano wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) uliofanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na Rais Magufuli.

Mwingine aliyevuma ni Wema Sepetu, msanii wa filamu ambaye alitangaza kujiunga Chadema mapema mwaka huu akisema CCM ilimtenga wakati alipopata msukosuko ulioishia kwa kukutwa na msokoto wa bangi na kufunguliwa kesi.

Wema, ambaye ni motto wa balozi wa zamani, na mama yake walihamia Chadema Februari 23 lakini mwezi uliopita amerejea CCM akidai anataka sehemu ambayo atapata “amani ya moyo”.

“Siwezi kuendelea kuishi kwenye nyumba inayonikosesha amani. Peace of mind is everything for me. Natangaza rasmi kuondoka Chadema na kurudi nyumbani…. #ThereIsNoPlaceLikeHome… Feels good to be Back,” aliandika katika akaunti yake ya Twitter.

Ndipo tetesi za wabunge zaidi kujivua nyadhifa zao zilipopamba moto na kuwalazimisha kujitokeza kuzikanusha. Hao ni pamoja na Saed Kubenea wa Ubungo (Chadema), Maftah Nauchuma (Mtwara Mjini, CUF) na John Mnyika (Kibamba, Chadema).

Ni mpango wa muda mrefu

“CCM imekuwa na kampeni ya muda mrefu ya kushawishi makada wa upinzani,” alisema Profesa Gaudence Mpangala, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa.

“Tumemsikia aliyekuwa mbunge wa Segerea, Dk Makongoro Mahanga akisema amekuwa akishawishiwa kuhama mara kwa mara. Kimsingi lengo la CCM ni kudhoofisha upinzani ili kiendelee kutawala.”

Alisema uteuzi wa viongozi wa upinzani kushika nafasi za serikalini ni moja ya mbinu za kuwashawishi wajiunge na CCM.

Alikuwa akimaanisha Dk Kitila na Mghwira walioteuliwa kwanza kushika nafasi za ukatibu mkuu wa wizara na ukuu wa mkoa kabla ya baadaye kutangaza kujiunga na CCM.

Pia alisema sababu nyingine ni mazingira magumu kwa wapinzani kuendesha siasa zao.

“Wale wasio na moyo wa kuhimili vishindo ni rahisi kuhama upinzani kwa sababu wapinzani wananyanyaswa kwa kukamatwa, kuwekwa ndani. Mtu anaona ili awe na amani ni bora tu ajiunge na CCM,” alisema Profesa Mpangala.

“Sioni kama ni njia bora ya kuendeleza demokrasia ya vyama vingi. Inatakiwa vyama vyote viwe sawa na uwanja wa ushindani uwe sawa.”

Hata hivyo, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Alexander Makulilo anasema tabia ya wanasiasa kuhama chama kimoja na kwenda kingine imekuwapo tangu mfumo wa vyama vingi uliporejeshwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, lakini hauwezi kuua upinzani.

“Ukiangalia Katiba ya Jamhuri ya Muungano na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 inazuia chama kumlazimisha mtu kujiunga nacho au kutumia mabavu, ulaghai au rushwa kupata wanachama. Zinaruhusu watu kuhama kwa hiyo sioni kwamba mfumo wa vyama vingi utakufa,” anasema Dk Makulilo.

Anataja sababu kubwa za kuhama kwa wanasiasa kuwa ni ni za kibinafsi ikiwa pamoja na kutafuta madaraka na kiujumla.

Akizungumzia madai ya kunyanyaswa wapinzani, Dk Makulilo anasema kama ni katazo la kufanya mkutano ya hadhara linaviathiri vyama vyote ikiwamo CCM na kwamba madai mengine yameshughulikiwa na vyombo vya kutoa haki.

“Kama ni tuhuma za rushwa bado zinashughulikiwa, siyo mwisho. Kupeleka ushahidi Takukuru siyo mwisho. Ndiyo maana hata aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Khamis amekamatwa hivi karibuni kwa tuhuma za rushwa na Rais Magufuli amejipambanua kupambana na rushwa,” alisema.

Dk Makulilo amewataka wanasiasa wa pande zote kuyasoma mazingira ya siasa ya sasa akisema yamebadilika, hivyo lazima wabadilishe mikakati ya kupambana.

Msaidizi wa Nyerere azungumza

Joseph Butiku, kada wa CCM na aliyewahi kuwa msaidizi wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Mwalimu Nyerere, amesema tabia iliyoibuka ya kuhamahama vyama inasababishwa na kutokuwa na msimamo.

Butiku alisema inaruhusiwa kulingana na roho ya mtu inavyopenda, lakini wakati mwingine kitendo hicho ni dalili ya kukosa msimamo.

“Watu wanatoka katika chama chenye msimamo, wanasema msimamo hapo haupo wanakwenda huko. Wakati mwingine wanatoa matusi mengi na kashfa ya huko wanakotoka. Wakifika wanasema huku ndio tumefika kubaya kabisa, wanarudi wanasema huku tulikotoka kumbe pazuri. Mimi nina shaka sana na watu wa namna hii lazima niseme,” alisema Butiku.

Butiku ambaye amekuwa msaidizi wa Mwalimu Nyerere tangu akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu, alisema hana hakika kama hao wanaorudi CCM wamejitathmini na wanakubaliana na misingi na misimamo waliyoikimbia awali.