24 wanusurika kifo mabasi yakigongana

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley

Muktasari:

Ajali hiyo imetokea jana saa 7:40 mchana katika barabara ya stendi kuu ya mabasi mjini Igunga

Tabora. Watu 24 wamenusurika kifo baada ya mabasi waliyokuwa wamepanda kugongana katika stendi kuu ya mabasi wilayani Igunga Mkoa wa Tabora.

Akizungumza leo Jumamosi Septemba 22, 2018 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema ajali hiyo imetokea jana saa 7:40 mchana katika barabara ya stendi kuu ya mabasi mjini Igunga.

Amesema basi la kampuni ya Salmin  lililokuwa likiendeshwa na Mohamed Sudi (28) liligongana na basi la kampuni ya Mghamba Express lililokuwa likiendeshwa Mahamoud Mohamed( 35).

Amesema basi  la Salmin lilikuwa likitoka stendi ya Igunga kwenda kijiji cha Loya wilaya ya Uyui  liligongana na  basi la Mghamba lililokuwa likiingia katika stendi hiyo.

Amesema majeruhi walitibiwa na kuruhusiwa na kwamba madereva wa mabasi hayo wanashikiliwa na polisi na Septemba 24, 2018  watafikishwa mahakamani.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya ya Igunga, Geofrey Cyril amesema waliwapokea majeruhi 24, wanawake 10 na wanaume 14 na wote walitibiwa na kuruhusiwa.