330,000 wavuliwa mikono ya sweta

Mganga Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Seif Mhina

Muktasari:

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Seif Mhina alisema hayo kwenye uzinduzi wa kondomu za ‘Zana ya Ukweli’ zinazosambazwa na Serikali kwa lengo la kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi.

Mbeya. Wanaume 329,000 wenye umri wa kuanzia miaka 10 na kuendelea wametahiriwa mkoani hapa, katika kampeni maalumu  ya ‘kuondoa masweta’ tangu mwaka 2012 hadi Juni ikiwa ni mkakati wa kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Mganga Mkuu wa mkoa huo, Seif Mhina alisema hayo kwenye uzinduzi wa kondomu za ‘Zana ya Ukweli’ zinazosambazwa na Serikali kwa lengo la kuzuia maambukizi mapya ya Ukimwi.

Kondomu milioni 21 zinatarajiwa kusambazwa nchini bure kwa watumiaji na atakayepatikana akiziuza atachukuliwa hatua kali. Dk Mhina alisema malengo ya tohara hiyo ni kuwafikia wanaume 410,000 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2012, Mbeya ilikuwa ikishika nafasi ya tatu kwa maambukizi na watu tisa kati ya 100 walikuwa na VVU.