
| ‘SMZ haitawaonea aibu waliosababisha meli kuzama’ | Send to a friend |
| Saturday, 28 January 2012 09:10 |
|
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar, imesema haitamuonea haya mtu yeyote aliyehusika katika uzembe uliosababisha kuzama kwa Meli MV Spice Islanders, Septemba mwaka 2011. Msimamo huo ulitolewa jana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, baada ya kupokea mchango uliotolewa na Uongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, kwa ajili ya watu walioathiriwa na tukio hilo. Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeanza kutekeleza kwa vitendo mapendekezo yaliyomo ndani ya ripoti ya tume iliyokuwa imeundwa na Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohamed Sheni, kuchunguza chanzo cha kuzama kwa meli hiyo. “Tayari wengi waliotajwa wameshachukuliwa hatua kwa mujibu wa mapendekezo ya tume,” alisema Balozi Seif. Alisisitiza kuwa ripoti kamili iliyotolewa na tume hiyo itawekwa hadharani muda si mrefu kupitia mitandao ya Internet ili kila Mwananchi apate fursa ya kuisoma kwa makini. “Kila mwananchi atapata nafasi ya kusoma ripoti hiyo muda mfupi tu baada ya kuiweka katika mtandao,” alisema. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania, Jumbe Menja, alisema uongozi wa taasisi hiyo uliguswa na tukio hilo la kihistoria katika visiwa vya Zanzibar . “Tukio lile kwa kweli limeweka historia mpya kabisa katika nchi yetu na huzini isiyosahaulikana miongoni mwa wananchi wa Tanzania ,” alisema Menja. Tayari baadhi ya vigogo wengi wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka yanayohusiana na uzembe uliosababisha meli hiyo kuzama baharini katika eneo la jirani na Kijiji cha Nungwi, katika Kisiwa cha Unguja. Meli hiyo ilikuwa inatokana Unguja kwenda Pemba. |













