MwanzoContactsEmail
Home Habari Habari za Kitaifa Wabunge CCM wataka Waziri wa Afya ajiuzulu
BOOKMARK THIS PAGE
Wabunge CCM wataka Waziri wa Afya ajiuzulu  Send to a friend
Saturday, 04 February 2012 09:02

Midraji Ibrahim, Dodoma
KAMATI ya wabunge wa CCM imemtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, Naibu wake, Dk Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, kujiuzulu kwa kile walichoeleza kuwa wao ni chanzo cha mgomo wa madaktari unaendelea nchini.Wakati hayo yakijitokeza, Bunge limejitosa kusuluhisha mgogoro huo kwa kusikiliza pande zote zinazohusika; Serikali na madaktari.

Pia, wabunge hao wa CCM wanadaiwa kuishutumu Serikali kwa kuchukua muda mrefu kabla ya kuingilia kati masuala muhimu ya taifa likiwamo hili la mgomo.Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho kilichofanyika juzi usiku, zimeeleza kuwa wabunge hao walidai kuwa viongozi hao wamekuwa kiini cha mgogoro wa madaktari kwa kushindwa kutoa suluhisho na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.

Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM), anadaiwa kuwa wa kwanza kutaka viongozi hao wajiuzulu na wakikaidi wawajibishwe na mamlaka husika yani Rais.

Pendekezo hilo liliungwa mkono na Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka aliyehoji hatua ya Serikali kuchelewa kutoa uamuzi kuhusu masuala ya kitaifa.Sendeka anadaiwa alituhumu Serikali kushindwa kuingilia kati haraka migogoro inayojitokeza nchini na kusubiri hadi maafa yatokee.

Kauli ya Serikali bungeni
Akiwasilisha kauli ya Serikali bungeni jana, Dk Mponda huku akitoa mlolongo wa historia ya mgomo huo, alisema Januari 30, mwaka huu, Serikali iliunda kamati ya kushughulikia maazimio yaliyowasilishwa na madaktari kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Dk Mponda alisema kamati hiyo itayachambua na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia Serikali kumaliza mgogoro huo wa watumishi wa sekta ya afya na kwamba, tayari imeanza kazi.

“Kamati hiyo inajumuisha wajumbe kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi), Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Wizara ya Fedha, Tughe, mwakilishi wa madaktari, mwakilishi wa wauguzi, Tamisemi, Mwanasheria Mkuu na Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Ajira,” alisema.Waziri Mponda alisema kamati hiyo imepewa hadidu za rejea zinazoainisha masuala yanayotakiwa kufanyiwa kazi na itafanya kazi kwa wiki mbili.

Hadidu za rejea zilizotolewa ni kupitia hali ya sasa ya maslahi ya madaktari na watumishi wengine wa kada za afya; kupitia, kufanya uchambuzi wa kina wa madai ya madaktari na watumishi wengine wa kada hiyo; kubaini gharama za utekelezaji wa madai ya maslahi ya madaktari na watumishi wengine wa sekta hiyo.

Nyingine ni kupendekeza na kushauri namna bora ya kushughulikia madai ya watumishi hao kipindi cha muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu na kuandaa taarifa na kuiwasilisha kwa Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii.

Awali, Dk Mponda alisisitiza kuwa mgomo huo siyo halali kwa sababu kisheria madaktari hawaruhusiwi kugoma.
“Masharti haya yanaainishwa katika kifungu cha 77 (1)(a) cha Sheria ya Ajira na Uhusiano kazini (Na.6 ya mwaka 2004) ambayo inazuia kugoma watumishi wote walio katika ‘huduma muhimu’ (Necessary Services),” alisema.
Dk Mponda alisema madaktari wapya wanaoajiriwa wanalipwa 957,700, huku watumishi wa kada nyingine kama wahandisi wanaanza na Sh600,000 na wahasibu wanaanza na mshahara wa Sh469,200.

Alisema utekelezaji wa pendekezo la madaktari la kulipwa mshahara wa Sh3.5 milioni kwa mwezi kwa daktari atakayeanza kazi, utalazimu Serikali kurekebisha viwango vya mishahara kwa watumishi wote wa afya na kada zingine na mhudumu wa sekta hiyo atakuwa analipwa Sh670,316 na mshahara wa juu wa kada hiyo utakuwa Sh8,145,573.

“Utekelezaji wa pendekezo hili utaigharimu Serikali Sh83,508,834,430 kwa mwezi ambayo ni sawa na Sh417,544,172,150 kwa kipindi kilichobaki cha miezi mitano mwaka huu wa fedha,” alisema.

Hata hivyo, Dk Mponda alisema hivi sasa hali ni nzuri isipokuwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi), ambako alidai wanawasiliana na Wizara ya Ulinzi na JKT kwa ajili ya kupeleka madaktari wanajeshi.

Kauli za wabunge
Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi), alisimama na kutumia kanuni ya 53 (a) ambayo inatoa ruhusu ya kutengua kanuni yoyote, huku akitaka kutengeuliwa kwa kanuni 49 (2) inayozuia kauli inayopelekwa na Serikali kujadiliwa bungeni.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), aliyesema kauli hiyo ni muhimu sana, inayohusu afya za Watanzania na sekta ambayo inatengewa fedha nyingi lazima ijadiliwe.
Awali, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (Chadema), akitumia kanuni ya 5 (1) na Ibara ya 63 (2), alitaka kanuni ya 49 (2) kutenguliwa kutokana na unyeti wa kauli hiyo.

“Serikali ni mmoja wa watuhumiwa kutokana na waziri, naibu wake na katibu mkuu kwa utendaji wao mbovu …itapelekea tushindwe kuijadili na tusiwawajibishe kwa ubovu wao,” alisema Mnyika.

Kauli ya Naibu Spika
Akitoa mwongozo wake, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema hoja hizo hazikuungwa mkono na wabunge kwa hiyo wanabanwa na kanuni zao, huku akiwataka watakapokuwa wazinafanya marekebisho kuangalia kanuni hiyo.

Hata hivyo, Ndugai alisema suala la mgomo wa madaktari ni zito na kwamba, tatizo lililojitokeza ni kusikiliza upande mmoja wa Serikali kwa sababu, madaktari hawawezi kwenda kusimama bungeni kueleza madai yao.

“Waziri ametueleza kuwa wameunda kamati ya kupitia madai ya madaktari,  nakumbuka mojawapo ya madai yao ambayo Serikali haikutaja hapa na hiyo nina uhakika hiyo kamati haitasema ni kwamba, Wizara ya afya kuna baadhi ya watendaji wenye uwezo wa kiutendaji wana kauli mbaya na dharau,” alisema Ndugai na kuongeza:

“Hiyo haimo. Uamuzi wa kuhusu jambo hili nalipeleka Kamati ya Huduma za Jamii, ilifanyie kazi haraka kwa kuita pande zote zinazohusika ziweze kueleza madai yao na tutapata mwafaka haraka.”


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #8 2012-02-09 17:44
Leo waziri Mizengo Pinda amefanya kazi ya kukutana na madaktari muhimbili na kutoa taarifa ya uwajibikaji ya Katibu wa afya na mwenzake mganga mkuu. Sasa bado yule waziri wa afya na yule mama wa kichaga Nkya nao wasombwe. Walichokwishaki chuma kimewatosha wakamalizie huko makwao. Tunataka watu wachapakazi kwenye wizara hii nyeti na sio wezi na waongo kama hao. Hivi wajue wakifa hawataenda ha chochote mbele ya haki na malipo ya mtu ni hapa duniani.

Rais tafadhali muwajibishe waziri wa afya na naibu wake mchaga. Vilio vimetikisa familia nyingi sababu ya hawa Chama Cha Tumbo Mbele. Waondoke kabisa.
Quote
 
 
0 #7 2012-02-06 11:06
NI KWELI KWAMBA NCHI YETU NI KISIWA CHA AMAN LAKIN KUNA BAADHI YA WATU WANATAKA KUSABABISHA AMAN HII IPOTEE KWASABABU SHERIA YA JAMHURI WA MUUNGANO WA TANZANIA IASEMA NO ONE IS ABOVE THE LAW(HAKUNA MTU YEYOTE YUKO JUU YA SHERIA)LAKINI KUUNA WATU HUSUSAN VIONGZI WETU AMBAO WANATUMIA MADARAKA KINYUME NASHERI LAKIN INAPO GUNDULIWA WATU HAO HAWACHUKULIWI HATUA HII NDIO ILE INALETA MADARAJA KATIKA JAMII KWA MFANO FIRST CLASS(DARAJA LA KWANZA NI VIONGOZ)SECOND CLASS(DARAJA LA PILI NI MWANANCHI WA KAWAIDA)HIVI KWELI HAPA SHERIA INATENDA HAKI.IPO HAJA YA VIONGOZI WETU KUMRUDIA MWENYEZI MUUNGU KWASABABU WANATANGULIZA MASLAHI BADALA YA KUMTANGULIZA MWENYEZI MUUNGU
Quote
 
 
+4 #6 2012-02-04 12:07
Mwaka 1994 wakti Watusi na Wahutu walikuwa wanauana wenyewe kwa wenyewe kwa siku 100 mfulilizo, Umoja wa Mataifa na AOU wakati huo walika kimya mpaka Kagame kafanya kazi nzuri licha watu millioni moja walikufa, leo hii Watanzania wanakufa kila siku mamia kwa mamia mahospitalini na Waziri Mponda na mwenzake Nkya wanasema tume inafanya kazi!!! aibu, tunaomba Kagame mwingine atoke hapa asaidie yaani Chadema, kwani vyama tawala CUF na CCM vimeshindwa kazi. Wanaokufa Gadafi aliwaita mende, sisi tuwaiteje wanaokufa kwa sababu ya uzembe wa utawala mbovu wa mawaziri wahusika!
Quote
 
 
+3 #5 2012-02-04 11:56
We mr Ndugai ni jiwe umethubutu tunakuaminia endelea kusimamia haki ya madokta na pia bunge sasa chini yako lianaonyesha dalili za kupenda wanyonge wanaodhulumiwa na serikali isiyojali raia wake.
Quote
 
 
+2 #4 2012-02-04 11:48
Ninaomba Watendaji wa Wizara ya Afya wanaotuhumiwa kwa utendaji mbovu wajiuzulu haraka sana.Hii itasaidia sana kutatua tatizo tulilonalo nchini la kumbeba mtu hata kama ni mbovu halafu kwa kufanya hivyo unahatarisha maisha ya watu wote.Hii ni mbaya sana.Na kama viongozi wetu hawataonyesha mfano mzuri wa kuwajibika jambo baya kama hilo itakuwaje huku chini?Wajibikeni jamai ili kuiponya nchi!!!
Quote
 
 
+3 #3 2012-02-04 11:40
Madaktari na wafanyakazi wote wa sekta ya Afya kwa ujumla waangaliwe maslahi yao. Tukumbuke kuwa kazi ya Afya inamtaka mtoa huduma hiyo wakiwemo madaktari, manesi na wengineo kuwepo kwenye kituo chake cha kazi muda wote tofauti na hizo kada nyingine ambazo watu huzunguka kukagua miradi kila leo na kujiingizia Per Diem. Ukitaka uhalisia wa hili angalia maisha ya Daktari mwenye Digree na mhasibu mwenye Certificate tu au hata hao wahandisi. Wakati hata Afisa Misitu mwenye ngazi ya cheti anapewa pikipiki na serikali lakini madaktari na manesi wameachwa watembee kwa miguu hata wale wanaoingia usiku. Hao madaktari wanaotoka Jeshini kazi zao huko wanakotoka anazifanya nani? Hiyo ni sawa na kutoa pesa mfuko wa kushoto na kuhamishiaa wa kulia na kujiona una pesa nyingi.
Quote
 
 
+3 #2 2012-02-04 10:11
Hawa wabunge wa CCM vichwa maji kweli, walikuwa wapi siku zote? Au yote hiyo ni kwasababu Mwenyekiti wao aliwakatalia posho? Inji hii kazi kweli
Quote
 
 
+4 #1 2012-02-04 09:44
waziri wa afya hajaongelea hoja nyingi za madai ya madaktali mojawapo ikiwa yeye mwenyewe kujihuzuru wazifa wake pamoja na rufaa za wabunge kwenda kutibiwa nje ya nchi hivyo waziri wa afya ,naibu waziri wa afya na katibu mkuu ni vyema wajihuzuru wameshindwa kufanya kazi kwenye wizara hiyo kwanza wana zarau na kauli mbaya
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner