
| Gari katika msafara wa JK lapinduka | Send to a friend |
| Friday, 18 June 2010 09:46 |
Anthony Kayanda, KigomaZIARA ya Rais Jakaya Kikwete mkoani Kigoma jana ilipata mushkeli baada ya gari moja kupinduka wakati msafari wake ukitokea Kibondo kuelekea Kigoma Mjini. Rais Kikwete, ambaye msafara wake umekuwa ukikumbwa na matukio ya hatari katika muda wa wiki tatiu, alikuwa anaenda Kigoma Mjini kuhitimisha ziara yake hiyo ya siku tatu mkoani hapa. Awali matukio mawili yaliyoukumba msafara wake yaliyuhusu magari ya Ikulu, likiwemo gari alilopanda wakati akiwa ziara ya wiki moja jijini Dar es salaam ambalo lilichomoka tairi muda mfupi baada ya kushuka, lakini ajali ya jana ilihusu gari la CCM mkoani Kigoma. Habari zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea jana asubuhi katika Kijiji cha Nyakitonto kilichopo wilayani Kasulu, umbali wa kilomita 25 kutoka mjini Kasulu. Kwa mujibu wa habari hizo moja kati ya magari yaliyokuwa katika msafara wa Rais Kikwete lilipinduka na hivyo kusababisha tafrani kwa magari mengine kadhaa yaliyokuwa kwenye ziara hiyo. Gari lililopinduka limetajwa kuwa ni Toyota Landcruiser lenye namba za usajili za T 826 BEW ambalo ni mali ya CCM Wilaya ya Kigoma Vijijini. Gari hilo lililokuwa linaendeshwa na Amrani Juma, lilimbeba mwenyekiti wa mkoa wa CCM, Azim Premji ambaye amepata majeraha machache. Ajali hiyo ilisababisha magari yaliyokuwa nyuma kwenye msafara huo, kusimama kwa ajili ya kutoa msaada wa haraka kwa mwenyekiti huyo aliyekuwa amebanwa upande ulioangukia gari hilo. Baadaye Premji, ambaye aliwahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini, alitolewa kwenye gari hilo na kuingizwa kwenye gari jingine la CCM la wilaya ya Kibondo lenye namba T 547 BEW na kuendelea na msafara. Wakati wote wa ajali na msaada huo, baadhi ya viongozi wa CCM walikuwa wanatiririka machozi kutokana na kuhofia hali ya mwenyekiti huyo na dereva wake, mashuhuda waliiambia Mwananchi. Akizungumza baada ya kutolewa ndani ya gari hilo mwenyekiti huyo alisema ajali hiyo imetokana na mwendo wa kasi wa msafara huo. “Nilikuwa namwambia dereva apunguze kasi ya gari… msafara ulikuwa na kasi na barabarani kulikuwa na vumbi jingi likitimka; tulikuwa kasi sana na ilipofika katika kona hapo eneo la ajali, gari lilimshinda dereva na kupinduka,” alieleza Premji. Katika hatua nyingine Rais Jakaya Kikwete ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma kuchukua hatua kali kwa watu wanaoharibu vyanzo vya maji na kuhujumu mabomba ya mradi wa maji. Agizo hilo alilitoa alipokuwa akizindua mradi wa maji ya kutega wa Amkongoro katika Kijiji cha Mahembe katika ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma. Alieleza kuwa halmashauri ni lazima iwe na sheria ndogo kwa ajili ya kuwabana watu wanaohujumu mradi unaohudumia vijiji sita vya Mahembe, Simbo, Msimbo, Chankabwimba, Kamara pamoja na Kasuku. Awali katika risala yake mwenyekiti wa bodi ya watumia maji, Yahya Hamza alisema kuwa licha ya kupunguza umaskini na magojwa ya mlipuko, maji hayo yatatumiwa na wengi katika miradi ya uzalishaji mali. Hata hivyo Hamza alitaja changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza mradi huo kuwa ni bei ya vifaa vya ujenzi kupanda, mabomba kuibiwa na kutobolewa na watu kutojitokeza kushiriki. Changamoto nyingine ni kilimo na ufugaji kufanyika katika chanzo cha maji na hivyo udongo kuingia katika vyanzo vya maji na kuchafua maji. |



Anthony Kayanda, Kigoma












Comments