Watu 40 wakamatwa kwa mauaji Serengeti

Muktasari:

Zaidi ya wakazi 40 wa Kijiji cha Mikomariro wilayani Bunda wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili.

Serengeti. Zaidi ya wakazi 40 wa Kijiji cha Mikomariro wilayani Bunda wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Jafari Mohamed leo Jumamosi Januari 13 amesema bado wanawasaka watu wengine kuhusiana na tukio la mauaji ya watu wawili wakazi wa Kijiji cha Remng'orori wilayani Serengeti jana Ijumaa.

"Tuliokamata ni wale walioshiriki yowe iliyosababisha mauaji ya watu wawili kwa kuwakata kwa mapanga kwa sababu ya mambo ya mashamba, tunaendelea kuwasaka wengine wanaodaiwa kuhusika kwenye yowe hiyo," amesema.

Katika tukio hilo Wegesa Gikene na Nyamhanga Gembo wakazi wa Kijiji cha Remng'orori waliuawa kwa kukatwa na mapanga na wakati wakiwa shambani.

Hata hivyo chanzo cha mgogoro huo ni mpaka wa wilaya za Bunda, Serengeti na Butiama ambao unahusisha eneo la ekari 3,535.

Katika ziara ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi wilayani Serengeti Novemba 29 mwaka jana wilaya hiyo ilimwomba kushughulikia mgogoro huo kwa kuwa unadaiwa umedumu toka mwaka 1947.