
| Tatizo CCM si sura wasema wapinzani | Send to a friend |
| Thursday, 14 April 2011 21:08 |
|
BAADHI ya viongozi wa vyama vya upinzani nchini, wameponda mabadiliko ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kwa madai kuwa tatizo la chama hicho ni mfumo na si sura za watu. Kauli hiyo inafuatia hatua ya Halmashauri Kuu ya CCM,kuthibitisha safu mpya ya uongozi wa Kamati Kuu na Sekretarieti ya chama hicho. Hata hivyo, safu hiyo haikujumuisha baadhi ya vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi na ambao wamepewa siku 90, wawe wamewaachia ngazi, vinginevyo watawajibishwa. Wakizungumza na gazeti hili juzi kwa nyakati tofauti, viongozi hao wa vyama vya TLP, UPDP, NCCR-Mageuzi na DP, walisema CCM bado ina kazi mzito.Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila, alidai kuwa tatizo la CCM ni Mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete. Mtikila ambaye alizuia kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana kutokana na kutotimiza masharti ya wadhamini katika mikoa 10, alisema mabadiliko ndani ya CCM si lolote kwa kuwa yanalenga katika kubadili sura tu, wakati mfumo ni ule ule. "CCM si chama cha wanachama, hakuna demokrasia pale. Katibu Mkuu wa sasa wa chama hiki amechaguliwa na Mwenyekiti wa CCM, hata hiyo kamati kuu nayo imechaguliwa na mtu mmoja tu," alisema Mtikila. Mtikila alidai kuwa matatizo ndani ya CCM yanasababishwa na mtu mmoja na kusisitiza kuwa hata hao waliochaguliwa, hawataweza kubadilisha kitu kwa kuwa watafuata maelekezo ya mtu huyo. "Sasa kama mtu kakuchagua unafikiri utashindwa kumfuata vile anavyotaka, akikanyaga mguu wa kulia na wewe utakanyaga hapo hapo," alisema Mtikila.Alidai kuwa mabadiliko ndani ya CCM, yanapaswa kufanywa katika maeneo nyeti zaidi ambayo hata hivyo, hakutaka kuyataja. Katibu Mkuu wa NCCR, Samwel Ruhuza akitumia msemo 'imejivua gamba' unaomaanisha kuwa CCM imeanza ukurasa mpya na viongozi wapya, alisema "nyoka akijivua gamba si anabaki nyoka tu, tatizo la CCM ni mfumo na si sura za viongozi wa sasa na wa zamani." Alisema kuondoka kwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba na nafasi yake kuchukuliwa na Wilson Mkama, hakuwezi kukinufaisha chama hicho kama kikiendelea kutumia mfumo ule ule. "Siwaombei mabaya kwa kuwa wakivurunda nchi nayo itayumba, sisi wote ni Watanzania, tatizo la CCM hawafuati miiko ya uongozi, Mkama anaweza kuwa kiongozi mzuri ila anaweza kushindwa kufanya kazi kwa sababu ya mfumo wa uongozi ulivyo," alisema Ruhuza. Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema, aliipongeza CCM kwa hatua hiyo lakini alionya kuwa isijaribu kuua upinzani na kwamba vinginevyo, haitafika mbali. "Sawa wamefanya mabadiliko, nawapongeza lakini kamwe wasijaribu kuua upinzani wataishia pabaya sana, watizame maslahi ya taifa na kuacha ubinafsi," alisema kada huyo wa zamani wa CCM, kabla ya kuhamia NCCR Mageuzi na baadaye TLP. Alisema hata hivyo mabadiliko hayo hayawezi kumfanya yeye arudi CCM.Mwenyekiti wa UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema mabadiliko ndani ya CCM, huenda yakawafanya wapinzani kuanza upya harakati za kuking'oa chama hicho madarakani. "Unajua uongozi wa CCM uliopita chini ya Makamba ulikuwa ahueni kwa wapinzani, ila tutatizama wa hao wanaokuja, Makamba ilikuwa rahisi sana kupambana naye, uongozi wa sasa ukifanya vizuri hali ya upinzani inaweza kuwa ngumu," alisema Dovutwa. Mwisho |
















Comments
CCM haijafanya lolote kuwaingiza Meghji na Makamba Jr katika uongozi, wapo kwenye mtandao wa Mafisadi.
HAKINA JIPYA CCM, JUA LA CCM LINAKARIBIA KUZAMA