|
Leon Bahati
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimekiri kuwa muda wa kuvuana gamba kwa nguvu tayari umefika, lakini mkakati huo utabidi usubiri hadi Februari au Machi mwakani. Chama hicho kimeeleza sababu za kuuvutia pumzi mchakato huo kuwa ni kukamilisha mchakato wa uundaji wa Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili ngazi ya Taifa kwa chama hicho, ambayo iko kwenye mchakato wa kuundwa.
Hayo yalielezwa jana Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama katika mkutano wake na waandishi wa habari ambako pia alisema, mipango ya namna tume hiyo itakavyoendesha shughuli zake, imekamilika na kilichobaki ni upatikanaji wa wajumbe wake 14. Kazi inayofanyika kwa sasa, alisema Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM (CC), imekuwa ikiandaa namna ya kupata majina ya watu watakaounda kamati hiyo ambao wanaonekana hawawezi kushawishika katika kupendelea.
Wajumbe hao pia hawapaswi kuwa na nyadhifa nyingine zozote zinazoweza kuingiliana mchakato wa kazi yao. Alisema vikao vya juu, Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) vitapitisha majina ya kamati hiyo katika vikao vyake vitakavyofanyika kati ya Februari na Machi mwakani. “Mara baada ya tume hiyo kupitishwa, itaanza kazi yake mara moja,” alisema Mukama kufuatia baadhi ya vyombo vya habari kueleza kuwa CCM imeshindwa kutekeleza uamuzi wake wa kujivua gamba ili kukisafisha dhidi ya kashfa za ufisadi zinazowaandama baadhi ya wanachama wake.
Dhana ya kujivua gamba ilipitishwa na Nec katika vikao vyake vilivyofanyika kati ya Aprili 10 na 11 mwaka huu kwa kuwataka wale wote wanaotuhumiwa kwa ufisadi kujiondoa wenyewe kwenye nafasi zao la sivyo chama kingetumia nguvu kuwaondoa. Akirejea maagizo ya Nec Mukama alisema “Viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wenyewe kwa maslahi ya chama. Wasipofanya hivyo chama kitawawajibisha mara moja.” Akieleza juu ya tathmini ya chama hicho kuhusu kujivua gamba kwa hiari, Mukama alisema; “Hali ilivyo hadi sasa takribani miezi saba ya azimio hili kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote wa chama chetu, ambao ni walengwa.”
Kwa sababu hiyo, akasema: “Bila shaka wakati sasa umefika kwa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika.” Kilichokifanya chama hicho tawala kuwa njia panda katika kutekeleza azimio hilo, Mukama anaeleza kwamba ni namna ambayo mpango huo utatekelezwa kwa haki na mtu asionewe. Alisema utaratibu huo utapaswa kufanyika kwa kutumia kanuni za chama hicho za uongozi na maadili, ambapo tayari NEC na CC wameridhia iundwe Tume mpya itakayofanya kazi hizo.
Katika ngazi ya Taifa, alisema itaitwa Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili ya Viongozi na ngazi nyingine kuanzia Mkoa, Wilaya na Tawi, zitaitwa kamati za kudhimiti nidhamu na maadili. Kulingana na mfumo huo mpya, Mukama alisema tume na kamati hizo zitakuwa na madaraka ya kumchukulia hatua za kinidhamu kiongozi yoyote yule katika ngazi husika pasipo haja ya kusubiri utaratibu wa vikao ndani ya chama. Alisema kazi hiyo itaweza kufanyika baada ya kukamilika kwa mchakato wa kuunda Tume ya Udhibiti wa Nidhamu na Maadili, ambayo mchakato wake unakamilishwa na Secretarieti ya NEC. Alipoulizwa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya baadhi ya wanachama wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) waliodaiwa kutaka kuasi chama, alikiri kuwa uchunguzi ulifanywa dhidi ya mienendo yao kulingana na malalamiko juu yao.
Alisema mmoja wa viongozi wa CCM mkoani Mara ndiye aliyewasilisha malalamiko hayo akituhumu kikundi kilichodaiwa kuongozwa na Hussein Bashe.
Katika uchunguzi huo, Mukama alisema walibaini kuwa kwenye mkutano uliofanywa na Bashe haukuwa na mikakati ya kufanya uasi ndani ya chama ila kulikuwapo na hitilafu zilizojitokeza kutoka kwa watu wachache. Mukama aliwahakikishia waandishi wa habari kuwa vikao hivyo vya juu vya CCM viliangalia mkanda wa video wa mkutano huo na kujiridhisha kuwa Bashe hakuendesha mambo kinyume na taratibu za chama.
Awali akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha NEC kilichofanyika Dodoma juma iliyopita, Mukama alisema kati ya maazimio yaliyotolewa na kikao hicho Aprili mwaka huu, azimio namba 27 “linahitaji kutekelezwa haraka iwezekanvyo.” “Dhana hiyo ya kukipatia chama chetu sura mpya ndiyo iliyopewa jina la kujivua gamba na sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa
imekwishatengeneza mpango wa utekelezaji wa maamuzi hayo,’’ alisema Mukama. Alisema katika kikao chake kilichomalizika juzi, NEC imeamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya chama walipaswa kujipima na kujitafakari wenyewe na ikibidi wachukue hatua jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa. ENDS
|
Comments
CCM NATAKA IFE MAANA HAINA MAANA YEYOTE ILE